JPM: Kuongoza nchi ni Msalaba


*Asema anazeeka kuliko JK kwa kazi ngumu
*Atakayejaribu kuvunja Muungano atavunjika

Celina Mathew

Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amesema anaonekana mzee kuliko Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa sababu kuongoza nchi ni kazi ngumu akieleza kuwa ana kazi kubwa kuulinda Muungano na kuonya mtu atakayejaribu kuuvunja kuwa atavunjika yeye.

Alisema hayo jana alipohutubia wananchi kwenye maadhimisho ya Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mji huo ambao ndio makao makuu ya Serikali jana ulipambwa na shamrashamra za siku hiyo, iliyojumuisha maelfu ya wakazi na wageni wa kitaifa na kimataifa kwenye uwanja huo, ambapo pamoja na mambo mengine ulipambwa na maonesho ya ndegevita.  

Huku akitoa mfano wa waasisi wa Muungano na marais wa awamu zilizomtangulia, katika hotuba yake iliyojaa utulivu, Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kuelezea namna viongozi hao walivyolinda Muungano.

“Kuongoza ni kazi ngumu, mimi nazeeka kutokana na majukumu na kazi niliyonayo, lakini mnamwona Rais mstaafu, Mzee Jakaya Kikwete anaonekana bado kijana kuliko mimi,” alisema.

Aliongeza: “Mimi na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein tutalinda Muungano vizuri sana kama viongozi waliopita, kama tulivyoapa kuulinda na akitokea mtu yeyote kujaribu kuuvunja atavunjika yeye.”

Akizungumzia umuhimu wa amani, Rais Magufuli alisema bila tunu hiyo, hakuna kitakachowezekana nchini na kwamba ili yote yafanikiwe, lazima Muungano ulindwe kwa kuhakikisha wanaenzi yaliyoachwa na viongozi waliopita.

“Mimi na Shein tutafuata nyayo za viongozi waliopita kulinda Muungano. Leo tunaposherehekea tutafakari tulikotoka, tuliko na tunakokwenda,” alisisitiza.

Aliwataka Watanzania bila kujali makabila wala itikadi zao, kuungana kuulinda Muungano ili jina Tanzania lidumu na uweze kusherehekewa miaka mingi ijayo.

“Tulinde na kudumisha Muungano ili jina la Tanzania lidumu, nafahamu tukishikamana kwa pamoja tutaweza na tutasherekea miaka mingi ijayo,” alisema Rais Magufuli.

Mafanikio

Rais Magufuli alisema miaka 53 ya Muungano imeshuhudia mafanikio makubwa na kujengwa kwa Taifa lenye nguvu.

Alisema hadi sasa Tanzania ni nchi ya amani na mipaka yake ni salama, hali inayoifanya kufanya mambo kwa kujiamulia yenyewe.

“Tumepata mafanikio kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii, uchumi umekuzwa na kukabiliana na umasikini na utegemezi hususan kwenye umeme, shule zimeongezeka, miradi ya maji imeboreshwa, demokrasia imepanuka, hivyo Tanzania ya sasa si ya mwaka 1964,” alisema.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni nchi kuheshimika kikanda, kibara na duniani, pia kushiriki kutafuta na kulinda amani.

Alisema wapo waliofanya kazi kuhakikisha mambo hayo yanafanikiwa kwa kuwa kuleta Muungano si jambo rahisi.

“Kuleta Muungano ni vigumu kwa kuwa hata kulinda ndoa zetu imekuwa vigumu, hivyo kulinda Muungano si jambo rahisi,” alisema akitania.

Alitaja baadhi ya waasisi waliosababisha kuzaliwa na kudumu kwa Muungano kuwa ni Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere, marehemu Shekhe Abeid Amani Karume na viongozi wa awamu zote zilizopita, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.

“Leo katika kuadhimisha Muungano huo hapa tuna Mama Maria Nyerere  na Fatma Karume, nawashukuru viongozi waliopita kwa kulinda Muungano hadi leo,” alisema.

Changamoto

Alisema licha ya mafanikio pia kuna changamoto zilizosababisha kuundwa kamati ya pamoja ambayo Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Seif Iddi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alisema viongozi hao wanafanya kazi vizuri huku akisisitiza Watanzania kuhakikisha wanashirikiana nao na si kuwaacha peke yao kwa kuwa suala la Muungano ni la kila mtu huku akiwataka kuchapa kazi kwa bidii.

Dodoma

Rais Magufuli alisema kwa mara ya kwanza sherehe hizo zimefanyika makao makuu ya Serikali, hivyo ni ishara kuwa imedhamiria kuhakikisha yanakuwa kule.

Alisema katika kuhakikisha hilo linatimia, awamu hii ya kwanza tayari watumishi 3,000 wamehamia Dodoma na wengine wanaendelea.

Aliongeza kwa mwaka ujao wa fedha zimetengwa Sh bilioni 200 kwa ajili ya mchakato huo wa kuhamia kwa wafanyakazi waliobaki kwa awamu ya pili na tatu.

Aidha, alisema kuna mambo yanaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa treni ya umeme kutoka Dar es Salaam- Dodoma, maboresho na ujenzi wa barabara, uwanja wa mpira na miundombinu ya maji.

“Tunafanya hivyo ili kuhakikisha tunajenga miundombinu mizuri kwa wananchi wa Dodoma na Serikali kwa ujumla. Leo tunaona wananchi wamejitokeza kwa wingi hii inadhihirisha Dodoma ni makao makuu ya nchi,”alisema.

Awali, Rais Magufuli alisema siku ya jana ilikuwa siku ya historia kwa Taifa, hivyo kila Mtanzania ajivunie kwa kuwa ni Siku ya Kuzaliwa Tanzania.

Alisema mwaka 1964 Taifa jipya lilizaliwa baada ya Karume na Nyerere kusaini na kuchanganya udongo wa nchi hizo mbili (Tanzania na Zanzibar) na hivyo kuleta Muungano.

Alisema huo ni udugu wa kihistoria ulio kwenye kushirikiana na mataifa mbalimbali katika masuala ya kibiashara na uhusiano mzuri ulioletwa na TANU na Afro Shiraz, ambavyo viliunganisha nchi hizi mbili.

Wakati akimkaribisha Rais Magufuli kuzungumza na Watanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema kilichoshuhudiwa jana ni tendo la kwanza la kihitoria kwa mkoa wake na kwamba ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Maadhimisho hayo yalifanyika mkoani humo kwa mara ya kwanza katika historia ambapo maadhimisho hayo yalipambwa na gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopita mbele ya Rais kutoa heshima, vikundi vya burudani ikiwamo muziki, halaiki, kwaya na ngoma za kiasili.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo