Majambazi wafunga barabara usiku, washambulia madereva


Abdallah Amiri, Igunga

IGP Ernest Mangu
KUNDI la watu zaidi ya 15 wanaosadikiwa kuwa majambazi wenye mapanga, nondo na marungu wamefunga barabara na kuteka madereva wa malori na maguta.

Tukio hilo lilitokea jana ambapo waliua dereva wa guta na kumjeruhi wa lori huku wakiwapora fedha na simu kwenye kijiji cha Igogo kata ya Nanga wilayani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa shida akiwa amelazwa wodi namba nane katika hospitali ya wilaya, mmoja wa madereva wa malori Ramadhani Bakari (34) mkazi wa Dar es Salaam, alisema alikuwa akitoka Mwanza kwenda Iringa.

Alisema lakini baada ya kufika Igogo saa 6.30 usiku alikuta majambazi hao wametega magogo katikati ya barabara itokayo Dar es Salaam kwenda Mwanza huku wakimwamuru ashuke.

Bakari alisema baada ya kushuka chini majambazi hayo yalimwamuru atoe fedha na simu, na wakati anajiandaa kutoa fedha majambazi hao walimshambulia kwa marungu na mapanga kichwani hali iliyosababisha aanguke na kupoteza fahamu.

Bakari alibainisha kuwa baada ya kupata fahamu, alijikuta yuko ndani ya gari lake huku milango imefungwa huku simu zake mbili na Sh 40,000 zikiwa hazionekani.

Hata hivyo, Bakari alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwahi  eneo hilo la Igogo kwani majambazi hao walitumia dakika 20 kuteka magari na kuongeza kuwa kama polisi wangechelewa majambazi hao wangefanya mauaji makubwa kwa madereva wa malori kutokana na kipigo walichotoa.

Mmoja wa ndugu aliyeuawa ambaye alijitambulisha kwa jina la Hassani alisema ndugu yake huyo, Charles Masanja alikuwa akitoka kata ya Nkinga akiwa na magunia ya mkaa kwenye guta lake na alipofika Igogo saa 6 usiku ndipo akakutana na masahibu hayo.

Akiwa na mwenzake, walikuta malori yametekwa wakasimama   lakini muda mfupi nao wakashambuliwa na kuporwa Sh 300,000   huku Masanja akikatwa panga shingoni na kupigwa nondo kichwani na polisi walipofika walimchukua yeye na mwenzake na kuwakimbiza hospitali ya wilaya ambako muda mfupi alifariki dunia.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya, Magongo Merchades alikiri kupokea majeruhi Masanja na Bakari saa nane usiku huku akisema wakati wakipewa matibabu, Masanja alifariki dunia na kwa uchunguzi wa awali, unaonesha kifo chake kilitokana na majeraha makubwa kichwani na shingoni na kuongeza kuwa Bakari bado amelazwa wodi namba 8 na hali yake bado ni mbaya.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, John Mwaipopo alithibitisha kutekwa kwa madereva hao huku akifafanua kuwa maroli yaliyotekwa ni manne na kwamba dereva wa guta kwa sasa ni marehemu kutokana na kujeruhiwa vibaya.

Aidha, Mwaipopo alisema hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali dhidi ya majambazi hao na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kukomesha vitendo kama hivyo visijirudie.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo