Lissu alia hotuba ya upinzani kuzuiwa


Mwandishi Wetu 

Tundu Lissu
MNADHIMU wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, amesema baadhi ya maneno ya hotuba za kambi hiyo kuzuiwa kusomwa bungeni ni kinyume na kanuni za mhimili huo wa Dola. 

Mbunge huyo wa Singida Mashariki amesema kwa mujibu wa kanuni hizo, inatakiwa msomaji hotuba kuachwa asome kwanza ndipo aelezwe kuwa baadhi ya maneno aliyosoma ni kinyume na kanuni, si kumzuia kusoma maneno yaliyomo. 

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alitoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku mbili tangu Msemaji wa Upinzani wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Ally Salehe kususa kusoma hotuba yake ya upinzani kuhusu wizara hiyo. 

Salehe alilazimishwa kuacha kusoma baadhi ya maneno yakiwamo yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na mgogoro wa CUF. 

Hali hiyo ilitokea baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kusimama na kupinga baadhi ya maneno aliyotumia kama “kila wizara imekiona cha moto, wamebanwa mpaka wamevunjwa mbavu” na kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeathirika vibaya na kisu cha ngariba kwa kukata bajeti yake.

Baada ya malumbano, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alitoa uamuzi  kuwa maneno yaliyoandikwa kuanzia ukurasa wa tatu hadi wa saba kwenye hotuba hiyo yasisomwe wala kurekodiwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge. 

Kauli hiyo ilimfanya Salehe kutoendelea kusoma hotuba yake na yaliyobaki anamwachia ngariba afanye anavyotaka. 

Akizungumza na gazeti hili, Lissu ambaye hotuba yake ya Wizara ya Katiba na Sheria ilipingwa na AG kutokana na kuwa na dosari, alisema hotuba ya Salehe haikurekodiwa, sambamba na yake kutokana na uamuzi wa Kiti cha Spika. 

“Kwa kilichotokea, maana yake hotuba hairekodiwi. Hata yangu sijui kama imerekodiwa, ngoja nisubiri nione kama wataniletea marekebisho. Wasiponiletea maana yake haijarekodiwa,” alisema Lissu. 

“Mambo yanayofanyika kwenye Bunge la Tanzania ni ya kigeni, hatujawahi kuyaona kwa kweli. Huu utaratibu wa kuzuia watu kusoma hotuba zao ni utaratibu mpya na haupo kwenye kanuni kabisa,” alisisitiza.

Alisema juzi wakati akisoma hotuba ya kambi hiyo ya Wizara ya Katiba na Sheria AG na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu, walimkatisha kwa zaidi ya dakika 15 lakini muda wake haukulindwa na Kiti. 

Alisema licha ya kuwa maneno hayo yanazuiwa, lakini kiundani wanalenga kuwasilisha ujumbe stahiki ikiwa ni pamoja na kuikosoa na kuishauri Serikali.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo