Marufuku kusafirisha mkaa wilaya hadi wilaya


Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imezuia usafirishaji mkaa kutoka wilaya moja hadi nyingine katika hatua ya kudhibiti misitu isiendelee kuteketea nchini, huku ikipiga marufuku usafirishaji mbao kutumia vivuli vya nyaraka za vibali.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akieleza kwamba mabadiliko hayo muhimu katika biashara ya mkaa yataanza Julai.  

Akifungua mkutano wa 24 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika hapa, Profesa Maghembe alisema:

“Hakuna vibali vya kuhamisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya wilaya husika kwa ajili ya matumizi ya Watanzania wanaohitaji nishati hiyo, lakini biashara ya mkaa ya kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam hadi Zanzibar ni marufuku.”

Waziri alilalamika: “Wamekata misitu yetu yote, mito yetu imekauka, tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji kwa sababu watu wengi huko nje wanataka mkaa wetu.

“Tanzania si shamba la bibi, wote watakaotoa mkaa eneo moja hadi lingine kinyume cha sheria watashughulikiwa kwa sheria ya uhujumu uchumi.”

Alifafanua, kwamba kwa upande wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga, vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha mkaa ambao utauzwa kwa vibali maalumu mikoani.

Alisema mkaa huo hautakuwa na athari za kimazingira kwa sababu utazingatia taratibu za uzalishaji endelevu.

Wakati huo huo, Waziri Maghembe alimwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kumhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu wa Wakala hiyo, Arjason Mloge.

Atatakiwa kutoka makao makuu ya Taasisi hiyo kwenda Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) mkoani Kilimanjaro na badala yake atafutwe mtu mwingine mwaminifu.

Alisema uamuzi huo unatokana na udhaifu katika usafirishaji wa rasilimali za misitu ndani na nje ya nchi, ukiwamo usafirishaji kwa kutumia vivuli vya vibali haramu.

“Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya saa sita mchana wa leo (jana) na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya uhamisho,” amesema.

Kwa uamuzi huo, alipiga marufuku kuanzia jana usafirishaji mazao ya misitu ndani na nje ya nchi kwa kutumia vivuli hivyo.

Aliongeza kuwa katika kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Viwanda ya Serikali hakuna gogo litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini, alisema Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 sehemu ya 21 (1) hairuhusu kuchunga mifugo kwenye hifadhi za Taifa, mapori ya akiba, mapori tengefu na hifadhi za misitu.

Aliwataka watumishi wa Maliasili kusimamia sheria hiyo pamoja na kutoa mwito kwa wananchi kuifuata kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Waziri Maghembe aliwaonya majangili   kuacha biashara hiyo haramu ambayo hailipi kwa sasa na badala yake wachukue trekta wakalime.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo