…RC Dar anusurika panga la vyeti


Mwandishi Wetu

Rais John Magufuli
WAKATI watumishi wa umma 9,932 wakiondolewa serikalini kwa kughushi vyeti huku wakinusurika kushitakiwa kwa jinai, Serikali imekwepa kuchunguza vyeti vya wanasiasa, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anayetuhumiwa kughushi vyeti.

Akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa vyeti vya watumishi hao mbele ya Rais John Magufuli jana katika ukumbi wa Chimwaga wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alitaja viongozi ambao vyeti vyao havikukaguliwa.

Kwa mujibu wa Angellah, ukaguzi huo uliobaini watumishi hao wakiwa na vyeti vya kughushi, haukuhusu viongozi wa kisiasa wakiwemo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya wala madiwani.

Angellah alifafanua kuwa viongozi hao hawakukaguliwa vyeti kwa kuwa sifa za uongozi wao ni kujua kusoma na kuandika.

Serikali imechukua hatua hiyo wakati tayari mashitaka dhidi ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, yakiwa katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka kwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

Katika mashitaka hayo, Jacob anamtuhumu Mkuu huyo wa Mkoa kwa kughushi vyeti vya kitaaluma huku akijua fika kuwa vyeti anavyotumia   si vyake.

Jacob amedai katika mashitaka hayo kuwa Mkuu huyo wa Mkoa, amekiuka sheria za nchi kwa kula kiapo cha utii na uaminifu mbele ya Rais kwa uhusika wa kughushi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Magufuli mbali na kutaka watumishi waliokutwa na vyeti vya kughushi kuondoka wenyewe kabla ya Mei 15, alizungumzia tatizo lingine la wafanyakazi hewa serikalini.

Alisema alipoingia madarakani, walifanya ukaguzi na kukuta watumishi hewa 19,706 na kuhoji hivi hakukuwa na mawaziri? Hakukuwapo makatibu wakuu na viongozi wengine?

“Tulijiuliza kwa nini tunalipa fedha nyingi za mishahara zaidi ya Sh bilioni 700 kila mwezi, posho, likizo, michango kwenye mifuko ya jamii, tukachukua hatua, hebu tujaribu kutafuta kweli hawa watumishi wapo?” Alisema.

Alisema uchunguzi ulifanyika na kubaini watumishi 19,706 hivyo kwa sasa linaendelea.

Rais Magufuli alisema wanapozungumzia watumishi hewa 19,706, walikuwa wakichukua Sh bilioni 19,848 kila mwezi za mshahara hivyo ilisababisha hasara ya Sh bilioni 238.2 kwa Serikali kwa mwaka.

“Tumewatoa wote hawa watumishi hewa, lakini najua bado wapo kama asilimia moja au mbili wale nao endeleeni kuwachambua vizuri,” alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kuondoa watumishi hao, mishahara kwa mwezi na matumizi yalipungua kutokana na vitu hewa vyote kuondolewa.

“Tulijiuliza sana kama tumepata watumishi hao hewa tulikuwa tunapandisha vyeo hewa, hivyo tukaona twende kwenye kazi ngumu ambayo nchi nyingi zimeshindwa kuitelekeza ya kuchambua wenye vyeti hewa,” alisema na kuongeza:

“Unakuta mtu ana cheti kumbe ni cha mdogo wake au marehemu, unakuta anakitumia, wakati kuna watu wanahangaika kutafuta ajira na wana vyeti vilivyokamilika kama hapa, kumbe serikalini yapo majamaa hayana hata vyeti.”

Rais Magufuli alisema ndiyo maana michakato hii yote inafanyika na anajua kuwa lazima kuna watu watachukia, kwa sababu ya kuwaondoa ambao wameghushi vyeti.

Alisema walioondoka watamchukia lakini hawana cha kufanya, maana ndio wameondoka na anajua wataendelea kumchukia, lakini ambao watapata nafasi hizo na wana sifa watamwombea.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo