Gwajima afutiwa kesi ya Pengo


Grace Gurisha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imefuta kesi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ya kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Sababu ya kufutwa kesi hiyo ni Serikali kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani kwa wakati.

Kesi hiyo ilifutwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kesi hiyo ilipokuja kusikilizwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.

Mkeha aliifuta kesi hiyo chini ya Kifungu cha 225 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kwa sababu katika miezi 14 ya kesi hiyo kusikilizwa mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ulipeleka shahidi mmoja.

Hakimu alifikia uamuzi huo, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo kuiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kusikilizwa, lakini hawakuwa na shahidi, hivyo kuomba ahirisho lingine.

Awali, Askofu Gwajima alikanusha tuhuma za kumtukana Askofu Pengo, baada ya kusomewa maelezo ya awali (PH) na Wakili wa Serikali, Maugo.

Maugo aliiambia Mahakama kuwa katika tarehe isiyojulikana kati ya Machi 16 na 25, Askofu Gwajima alitoa mahubiri kwa wafuasi wake, kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Dar es Salaam.

Alidai wakati akitoa mahubiri hayo alitoa maneno ya matusi na ya kumfadhaisha Askofu Pengo, kuwa yeye ni mtoto, mpuuzi na mwenye akili ndogo sijui amekula nini? Mpuuzi yule, mjinga yule na yeye kuwa anaitwa Askofu Gwajima.

Wakili huyo alibainisha kuwa Askofu Gwajima wakati anatoa maneno hayo alirekodiwa kwa video na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati kesi hiyo inasikilizwa, Mahakama hiyo ilikataa kupokea CD na picha kama kielelezo cha kesi hiyo kwa sababu upande wa Jamhuri ulishindwa kutimiza vigezo vya kisheria kuwasilisha vilelezo vya elektroniki mahakamani.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, naye alipinga kupokewa kwa CD hiyo kwa madai kwamba shahidi aliyekuwa anawasilisha hakustahili kwani siye aliyeitengeneza CD hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo