Wanaodaiwa kuiba mafuta ya ndege kizimbani leo


Grace Gurisha

ASKARI wawili wanaotuhumiwa kuiba lita 280.6 za mafuta ya ndege wakiwa na watu wengine wawili leo wanatarajiwa kupandishwa kizimbani mara ya pili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi yao itakapotajwa.

Askari hao ni F.8419 Koplo Bahati Msilimini (33), F.9901 Konstebo Benaus (34), na wengine ni Iddy Nyangas (42) mlinzi wa kampuni ya Moko na Ramadhani Mwishehe (52) fundi wa ndege, wote wakazi wa Dar es Salaam.

Watu hao wanaoshitakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi wanatarajiwa kufikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Nassoro Katuga atatakiwa kuiambia Mahakama hatua ya upelelezi ilipofikia.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa mawili ya kula njama na hujuma wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Ilidaiwa katika mashitaka ya kwanza ya kula njama, kwamba  katika tarehe tofauti kati ya Machi mosi na 17 mwaka huu, walikula njama ya kutenda kosa la hujuma.

Katuga alidai katika mashitaka la pili kwamba, kati ya tarehe hizo wakiwa kwenye uwanja huo, walifanya hujuma dhidi ya Serikali kwa kuhujumu maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alidai walitoboa na kuchota mafuta ya ndege lita 280.6 kutoka ndege namba 5H-MWF.DASH 8 Q 300. Baada ya kusomewa mashitaka, hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

“Hamtatakiwa kujibu chochote kwa sababu makosa yenu ni ya uhujumu uchumi na pia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hajawasilisha mahakamani hati ya kuitaka Mahakama hii isikilize kesi hii,” alisema Nongwa.

Washitakiwa wako nje kwa dhamana ya wadhamini wawili ya Sh milioni moja na pia walitakiwa kutotoka nje ya nchi bila kibali pia kutosogelea eneo walilokuwa wakifanya kazi bila kibali.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo