5 mbaroni kwa vurugu za CUF


*Wadaiwa kuvamia kwa silaha mkutano wa wanahabari
*Mutungi aonya wanachama waheshimu kesi ya utata

Abraham Ntambara

Kamansa Simon Siro
SAA tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza kushikilia watu watano.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona  Polisi haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.

Viongozi hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.

Jumamosi iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.

Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.

Katika ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya Dola viko kimya.

“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.

Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”

Alisema baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni  wakapatanishwe.

“Tulishangazwa na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.

Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.

“Tulimwonya Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi hao,” alisema.

Sirro

Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watano wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.

“Tulipata taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na kukamata watu watano,” alisema Sirro.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.

Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.

Msajili aonya 

Pamoja na CUF upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ikimtuhumu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa kuchochea mgogoro unaoikabili, mwenyewe amewataka wanachama hicho kuheshimu kesi ya utata wa uongozi inayoendelea mahakamani.

Kupitia taarifa yake yenye kichwa cha habari ‘Kulaani vurugu zilizotokea katika mkutano wa wanaosemekana kuwa viongozi wa CUF na waandishi wa habari’, Jaji Mutungi alisema uwepo wa kesi mahakamani hauwapi mamlaka wanachama hao kufanya vurugu.

“Ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa haviko juu ya sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu tulionao,” alisema.

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja siku mbili tangu watu waliotumia gari lilikokuwa na nembo na bendera za CUF, kuvamia mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na viongozi wa chama hicho wilaya ya Kinondoni.

Katika tukio hilo, watu hao walipiga wanahabari na viongozi hao huku mmoja wa wavamizi aliyejifunika uso kininja, akichomoa bastola kutishia na mwingine akishindwa kuondoka na kushushiwa kipigo na wananchi.

Juzi upande wa Maalim Seif ulimtuhumu Mwenyekiti wa Chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuhusika na vurugu hizo, tuhuma ambazo zilikanushwa na wanaomuunga mkono.

Katika maelezo yake, Jaji Mutungi alisemaa suala la mgogoro wa uongozi katika CUF liko mahakamani, hivyo akiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na mlezi wa vyama hivyo anakisihi chama hicho kutambua kuwa uwepo wa shauri mahakamani, si fursa ya kufanya uvunjifu wa amani.

“Jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii. Ninalaani vurugu hizo ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu,” alisema.

“Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yako mahakamani, hebu tuheshimu utawala wa sharia,” alisema.

Alisema ofisi yake na Jeshi la Polisi wanashughulikia malalamiko yoyote kuhusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa, hivyo hakuna haja ya wanachama wa CUF kukiuka taratibu za kuendesha chama hicho na kujichukulia sheria mkononi.

Jaji Mutungi alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kufanyia kazi tukio hilo ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo