Shikuba, wenzake kupinga kukaa kizuizini


Mwandishi Wetu

Ali Hatibu Haji ‘Shikuba'
WAFANYABIASHARA watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, akiwamo maarufu Ali Hatibu Haji ‘Shikuba’, wanatarajia kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya kuwekwa kizuizini kusubiri kupelekwa Marekani kushitakiwa.

Watuhumiwa wengine ni Idd Mfuru na Tiko Emmanuel, ambao wote ni Watanzania, lakini wanahitajika Marekani kutokana na tuhuma za biashara za dawa za kulevya zinazowakabili.

Hatua hiyo ilifikiwa na mawakili wa wafanyabiashara hao, Hudson Ndusyepo na Majura Magafu, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kukubali maombi ya Waziri wa Sheria na Katiba ya kuwasafirisha Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa hizo.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Wakili Ndusyepo alisema lazima leo wakate rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huo kwa sababu tayari Mahakama ya Kisutu imekubali kusudio lao la kukata rufaa, kwa hiyo wanachosubiri ni mwenendo wa maombi hayo.

“Tungekuwa tumeshakata rufaa, lakini bado mwenendo wa kesi ulikuwa bado haujamalizwa kuchapwa, kwa hiyo kesho (leo) watamalizia na siku hiyo hiyo tutakwenda Mahakama Kuu kwa sababu wateja wetu wako mahabusu hivi sasa,” alisema Ndusyepo.

Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha alikubali washitakiwa wasafirishwe Marekani na akaamuru wakae rumande hadi Waziri wa Sheria na Katiba atakapopata kibali cha kuwasafirisha.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki kuwasilisha maombi hayo. Wakati maombi hayo yanasikilizwa, Kakolaki alidai kuwa yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili wa Serikali Msaidizi wa Marekani Texas, Richard Magnes ambacho kilithibitishwa na kuapwa kwa Jaji Nancy Johnson.

Kiapo hicho kinaeleza watuhumiwa hao walivyoshiriki katika mashitaka hayo, ambapo katika ushahidi, inaelezwa kuwa kuna mtu alikuwa amepandikizwa kuchunguza jinsi wanavyoingiza dawa za kulevya Marekani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo