Upumzike kwa amani Mwalimu Chrysostom Rweyemamu


Mashaka Mgeta

Chrysostom Rweyemamu
MWAKA 2006 nilipojiunga katika kampuni ya New Habari House (2006) Limited, nikiajiriwa kuliandikia gazeti la Mtanzania, nipo nilipokuwa karibu na mmoja wa waandishi nguli wa habari nchini, Chrysostom Rweyemamu.

Mei 28, mwaka huu, Rweyemamu aliyekuwa pia Mjumbe wa Bodi na Katibu mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), alifariki akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Wapo wanaoweza kukiona kipindi cha kuanzia 2006 nilipomfahamu Rweyemanu hadi sasa ni miaka michache. Hawatakuwa wamekosea kutokana na ukweli kwamba tafsiri ya namba inatokana na ufafanuzi wa anayejenga hoja.

Lakini pia katika utumishi wangu, sikudumu kwa muda mrefu kwenye kampuni hiyo. Nilifanya kazi kwa takribani mwaka mmoja, nikarejea katika kampuni ya The Guardian Limited niliyokuwapo kabla ya kujiunga New Habari House (2006) Limited.

Bado kuwapo katika kampuni hiyo kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja kinaweza kuonekana kuwa kifupi. Dhana hiyo inaweza kuwa sahihi kutokana na hoja inayojengwa na mtu anayeamini hivyo.

Hata hivyo, kuwa kwangu karibu naRweyemamu hakukuwa ndani ya kampuni hiyo pekee, bali katika ziara kadhaa zilizoandaliwa na JET kwenda kwenye maeneo tofauti ya nchi, kutathimini na kuandika habari zinazohusiana na mazingira.

Ninakumbuka katika ziara hizo, ukiacha maelekezo ya kitasnia, Rweyemamu alifahamika zaidi kwa utani uliotokana na kupenda kwake kutumia pilipili iluyowekwa kwenye chakula. Alipenda kutumia pilipili yenye ganda jekundu.

Ndio maana tulipofika hotelini, aliulizia aina ya pilipili iliyopo. Wakati mwingine alilazimika kwenda kununua pilipili nyekundu, ili mradi kukidhi hitaji lake.

Ziara hizo zinaweza kutafsiriwa kufanyika katika siku chache. Anayetafsiri hivyo anaweza kuwa sahihi kwa kadri anavyozifafanua hesabu zake na sababu zake.  

Ingawa ni hivyo, ukweli unabaki kwamba mimi ni miongoni mwa watu hususani waandishi wa habari waliobahatika kukaa, kufanya kazi, kula na kunywa pamoja na Rweyemamu.

Katika siku zangu za awali kujiunga New Habari House (2006) Limited, tofauti ya kwanza niliyoiona na mahali nilipotoka, yaani The Guardian Limited ni kuwapo kwa mafunzo ya ndani kwa waandishi wa habari.

Kwa kawaida, waandishi wa habari hukutana asubuhi kwenye chumba ama eneo maalum ndani ya chumba cha habari, kusoma, kujadili, kutathmini na kufanya ulinganifu wa habari zilizotolewa na chombo chao, ikilinganishwa na ilivyo kwa vyombo vingine.

Kisha waandishi hushiriki kutoa mawazo ya habari mpya, namna ya ukusanyaji wa taarifa, vyanzo vya kupatikana kwake (taarifa) na mambo mengine yanayohusu ratiba ya siku husika.

Lakini kwa New Habari House (2006) Limited hali hiyo ilikuwa tofauti kidogo. Kwamba kila Ijumaa hapakuwa na patio la magazeti, bali waandishi walikusanyika kwenye chumba mahususi kwa ajili yakushiriki semina fupi ya kukumbushana mambo ya kuzingatia katika uandishi wa habari.

Darasa hilo liliratibiwa na kuongozwa na Rweyemamu tunayeomboleza kifo chake sasa. Rweyemamu alimudu kutumia taaluma na uzoefu wake katika tasnia ya habari kufundisha, kukumbusha na kuelekeza namna bora ya kuandika habari zenye maslahi kwa umma.

Rweyemamu alikuwa muumini mzuri wa matumizi sahihi ya lugha hasa za Kiswahili na Kiingereza. Licha ya kuchapisha gazeti la Mtanzania, New Habari House (2006) Limited ilikuwa (nafikiri hadi sasa) ikichapisha gazeti la The African kwa Kiingereza.

Namna bora ya ufundishaji, uelekezi na ushirikishi wa Rweyemamu kupitia darasa hilo, yalinifanya nijione ‘kiumbe mpya’ katika tasnia ya habari, nikipata ujuzi zaidi, uelewa zaidi na ufahamu zaidi kuhusiana na masuala mbalimbali ya uandishi wa habari.

Ninatambua na wengine wengi wanaweza kulikubali hili, kwamba katika utendaji kazi wa uandishi wa habari, ni rahisi kugundua na kukosoa upungufu kadha wa kadha unaotokea, ukifanywa na waandishi wa habari.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Rweyemamu katika uhai wake. Alikuwa mwepesi wa kubaini upungufu katika uandishi wa habari kwa magazeti ya ndani ya New Habari House (2006) Limited nay ale yaliyokuwa yanachapishwa na kampuni washindani.

Ni kutokana na hali hiyo, nilijifunza na kupata uelewa mpana zaidi katika masuala ya uandishi wa habari hasa wa kivitendo kutoka kwa Rweyemamu aliyekuwa Mhariri, Mwalimu, muelekezi na msimamizi bora wa mafunzo ya ndani ya chombo cha habari.

Katika kuonesha dhamira nzuri ya kuleta mageuzi na mabadiliko chanya, Rweyemamu aliweka mfumo unaotoa fursa kwa kila mwandishi wa habari kunufaika kutokana na mafunzo hayo.

Mfumo huo ulihusisha kuwapo orodha maalum ya mahudhurio aliyoisimamia na kuhakikisha kwamba mafunzo ya ndani yanakuwa sehemu ya vigezo muhimu vya ushiriki wa mwandishi wa habari katika ajira yake.

Nilipenda kuwapo kazini kila siku kwa kadri ya hitaji la ajira yangu, lakini nilipenda zaidi kufika ofisi kila Ijumaa ili nisikose kipindi cha mafunzo yaliyotolewa na Rweyemamu.

Ndio maana, hata niliporejea The Guardian Limited baada ya takribani mwaka mmoja, miongoni mwa mambo niliyohisi kuyakosa, nikabaki ninayakumbuka ni kipindi cha mafunzo ya ndani kilichokuwa kinaongozwa na Rweyemamu.

Hata nilipokutana naye kwenye ziara za JET, Rweyemamu alikuwa na hulka ya kushirikiana na washiriki wote, waandishi wabobezi na hata waliochipukia katika tasnia hiyo.

Hakuwa na ‘uchoyo’ wa kutaka aonekane kuandika makala bora kuliko wengine, bali alishirikishana na waandishi wengine na kujadiliana masuala ya muhimu yaliyoibuka wakati wa ziara.

Ni nadra kuzikuta karama hizo kwa waandishi wengi ndani ya mataifa yanayoendelea, lakini Rweyemamu aliiishi hali hiyo na kuacha kizazi cha waandishi bora wa habari, wakiwamo wale waliopitia taasisi ya mafunzo ya uandishi wa habari ya Maarifa (Mamet) iliyokuwa chini ya kampuni hiyo.

Mwenyezi Mungu ampumzishe katika usingizi wa amani Chrysostom Rweyemamu-AMINA
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo