Ubani ajali ya wanafunzi wahojiwa bungeni

Sharifa Marira, Dodoma

SAKATA la fedha zilizochangwa kwa ajili ya kuwafariji wafiwa wa watoto,walimu na dereva wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha waliofariki katika ajali  kutumika katika matumizi mengine limetinga bungeni huku wabunge wakilaani.

Suala hilo limeibuka jana baada ya kipindi cha maswali na majibu ambapo Mbunge wa Ukonga,Mwita Waitara (Chadema) alitaka kupata mwongozo wa Mwenyekiti Andrew Chenge aliyekuwa anaongoza mkutano huo kuhusiana na taarifa ya fedha za rambirambi kupelekwa kukarabati hospital ya Mount Meru iliyopo Arusha.

‘’Mheshimiwa Mwenyekiti naomba mwongozo wako kwa kutumia kanuni ya 68 (7) inayohusu jambo lilijitokeza mapema bungeni,Nilikuwa hapo nje nimeangalia magazeti yanaelezea matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya rambirambi na kuwafariji wafiwa wa watu waliofariki katika ajali ya shule ya Lucky Vincent zimetumika kinyume na malengo yake’’alisema Waitara na kuongeza kuwa

“Madaktari wamelipwa kama posho na fedha zingine  zinakarabati hospitali ya Mount Meru tofauti na ilivyokusudiwa,katika hili  bunge linahusika kwa maana tulikatwa posho hapa ili kusaidia familia za wafiwa,ilikuwa misaada klwa wahusika sasa hii tabia imekuwa ikijirudia.”

Alisema watu wamekuwa wakichanga kwa ajili ya kusaidia watu wanaopata matatizo lakini serikali imekuwa haifikishi fedha hizo kwa wahusika,tabia hiyo imekuwa ikijirudia  mara kwa mara jambo ambalo si zuri kwani watu wataacha kuchanga wakijua kwamba fedha hazisaidii walengwa.

“Tabia hii inanikera hata mimi mwenyewe kama tutakuwa tunachanga fedha za rambi rambi alafu inabadilishwa matumizi juu kwa juu bila hata wahusika kupelekewa,kama ni hivyo ni vyema kila chama kikakusanya fedha za michango wenyewe au kada zingine zifanye hivyo kwa lengo la kuwafikishia wahusika wenyewe ili kuepuka ulaji wa fedha za michango’’

Akijibu mwongozo huo,Chenge alisema “Kwa mila na desturi za kiafrika ukishatoa mchango wako wa rambi rambi unawaachia familia ile au chombo kile,sijatoa  mwongozo  haya ni maoni yangu,naomba tusiendeleze jambo hilo,serikali ipo bunge lipo unategemea mrejesho ili siku nyingine mkiombwa iwe rahisi kutoa lakini kuleta tuhuma tu sio”

“Ila kwa mwongozo wangu swala lako halijatokea mapema bungeni leo kwahiyo sina cha kulijibia,hatuendeshwi na magazeti humu bungeni.”

Mchango uliotolewa na bunge kwa ajili ya kuwafariji wafiwa ni milioni 100 ,michango ya jumla iliyotolewa na wadau ni zaidi ya milioni 300 ambapo fedha zilizotolewa kwa familia za wafiwa ni zaidi ya shilingi milioni 133 ambazo  katika wafiwa 35 kila familia ilipata shilingi milioni 3.8.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo