Pingamizi la Shikuba wa dawa za kulevya Mei 28


Grace Gurisha

WAKATI kukiwa na mkanganyiko kuhusu  wapi walipo watuhumiwa wa dawa za kulevya akiwamo mfanyabiashara maarufu Ali Hatibu Haji maarufu Shikuba na wenzake, Mahakama Kuu inatarajia kusikiliza pingamizi la washtakiwa hao la kukataa kupelekwa Marekani, Mei 28, mwaka huu.

Watuhumiwa wengine ni Idd Mfuru na Tiko Emmanuel. Pingamizi hilo linatarajiwa kusikilizwa na Jaji Sawaji wa mahakama hiyo na washtakiwa watawakilishwa na Wakili Majura Magafu na Hudson Ndusyepo.

Magafu na Ndusypo walifikia hatua ya kukata rufaa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutoa uamuzi kuwa wanapinga uamuzi wa kukubali maombi ya Waziri wa Sheria Katiba ya kuwasafirisha Shikuba na wenzake kwenda Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Hata hivyo, wakati wanasheria hao wanasubiri rufaa yao ipangiwe tarehe na Jaji wa kusikiliza pingamizi hilo, kuna taarifa kuwa Shikuba na wenzake wamesafirishwa kwenda Marekani.

Hali hiyo ilisababisha mkanganyiko kutokana na kwamba, tayari watuhumiwa walipeleka pingamizi Mahakama Kuu na kabla ya kusikilizwa wakaondolewa nchini, kwa hiyo tarehe hiyo ndiyo itajulikana kama wapo nchini au la.

“Mei 28 mwaka huu ndiyo Mahakama itatueleza kama wateja wetu wapo nchini au la kwa sababu hata sisi tumesikia wateja wetu wamesafirishwa tayari,” alisema Ndusypo akizungumza kwa njia ya simu na JAMBO LEO

Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha alikubali washtakiwa hao wasafirishwe kwenda Marekani na pia aliamuru wafanyabiashara hao wakae rumande hadi Waziri wa Sheria na Katiba atakapopata kibali cha kuwasafirisha.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki kuwasilisha maombi hayo.

Wakati maombi hayo yanasikilizwa Kakolaki alidai kuwa maombi hayo yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili wa Serikali Msaidizi wa Marekani Texas, Richard Magnes ambacho kilithibitishwa mbele ya Jaji Nancy Johnson.

Kiapo hicho kinaeleza watuhumiwa  walivyoshiriki katika mashtaka hayo na  katika ushahidi inaelezwa kuna mtu alikuwa amepandikizwa kuchunguza namna  wanavyoingiza dawa za kulevya Marekani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo