Madiwani 4 CCM wasimamishwa


Ibrahim Yassin na Moses Ng’wat, Kyela

KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mbeya imewasimamisha na kupendekeza kuvuliwa uanachama, madiwani wanne wa chama hicho, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kutokana na utovu wa nidhamu.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zilieleza jana kuwa, uamuzi huo ulifikiwa juzi baada ya madiwani hao kugomea kikao cha
Kamati ya Maadili na Uongozi wa Chama Mkoa, hali iliyosababisha suala hilo kupelekwa katika Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mbeya na kufikia uamuzi huo.

Mgogoro wa madiwani hao na Mwenyekiti wao umefukuta kwa muda mrefu jambo lililosababisha madiwani 19 wa CCM wakishirikiana na wenzao 12 wa Chadema, kumwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Musa Mgata, ili kuitisha Baraza Maalumu, kwa lengo la kumng’oa Mwenyekiti wao baada ya kukosa imani naye.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya kikao hicho kilieleza kuwa,  madiwani  hao wanne waliosimamishwa na Kamati hiyo ya siasa Mkoa na kupendekeza kuvuliwa uanachama ni  Lameck Mwambafula (Bujonde),  Fyuda Msusi  (Katumba, Songwe), Emmanuel Mwandambo (Ndandalo) na Furaha Mwasongela (Mababu).

“Mgogoro huu umesababisha shughuli zote za Halmashauri kusimama, vikao zaidi ya vitano vya Baraza vimeitishwa na kila wakifika wanagomea, lakini posho wanasaini… na ukiangalia wote hawa ndio vinara,  ndiyo maana nafikiri wajumbe wameona waondolewe,” kilieleza chanzo hicho.

Chanzo kingine kilieleza kuwa, mapendekezo hayo tayari yamewasilishwa katika ngazi ya Taifa ambapo baadaye yatafikishwa katika Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa ajili ya kuhitimisha suala hilo baada ya kupitia mapendekezo ya Kamati ya siasa Mkoa.

Hata hivyo, viongozi wa chama hicho ulipoulizwa juu ya taarifa hizo za kusimamishwa na kisha kupendekeza kuvuliwa uanachama madiwani hao, hawakukubali wala kukataa na badala yake walisema suala hilo mchakato wake bado unaendelea.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Willson Nkambako licha ya kukiri kushughulikia suala hilo, alisema  mchakato wake haujakamilika kwa ajili ya vyombo vya habari na umma kujua kila kitu.

“Kweli kikao kilikuwepo na kilishughulikia masuala ya ujenzi wa chama na suala hilo la Kyela lilikuwa linaendelea kusuluhishwa,”
alisema Nkambako.

Hata hivyo, Katibu huyo aliwataka waandishi wa habari kumtafuta katibu Mwenezi wa Chama hicho ili kupata taarifa zaidi juu ya sakata hilo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, alisema mapendekezo yote juu ya uamuzi wa kikao cha Kamati ya Siasa yamewasilishwa ngazi ya juu kwa ajili ya kuhitimisha suala hilo.

Mgogoro huo unadaiwa kuibuka baada ya kusimamishwa kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo, kutokana na tuhuma za ubadhirifu katika fedha za ushuru wa zao la kakao, Sh milioni 733.

Watendaji hao waliosimamishwa ambao hata hivyo walisharudishwa kazini ni Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Arafa Baraza na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Salome Lyimo waliosimamishwa kupisha uchunguzi.

Mwingine aliyesimamishwa ni Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo, Joseph Sengelema, kwa kinachodaiwa ni kutoa taarifa za uongozi juu ya ufisadi wa fedha hizo.

Hata hivyo, hadi sasa bado hajarudishwa kazini, licha ya tume iliyoundwa kubaini kuwa hana kosa, kutokana na madiwani kuendelea kugomea vikao vya mabaraza, ambavyo ndivyo vyenye mamlaka ya kumrudisha.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo