Matumizi ya silaha sasa yatiliwa shaka



Suleiman Msuya

IGP Mangu
WADAU wa amani nchini wametaja sababu sita za matukio yaliyohusisha matumizi ya silaha kwa siku za karibuni kuongezeka.

Wananchi hao wanaoamini katika amani wakiwamo wasomi, wanasiasa na mwanajeshi mstaafu, wametaja sababu hizo wakati Taifa likishuhudia matukio yanayohusisha silaha za moto kutishia, kujeruhi hata kupoteza maisha ya watu.

Katika matukio hayo, askari na wananchi wametishiwa kwa silaha wakiwamo viongozi wa kisiasa, pia askari na wananchi kuuawa hasa mkoani Pwani ambako watu wanaotuhumiwa kwa ujambazi hata askari, wamekuwa wakitumia silaha kutishia wananchi wasio na silaha.

Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya Rufiji, Kibiti na Mkurunga mkoani Pwani na askari kumtolea silaha aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akitaka kuzungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam.

Wakati aliyemtishia silaha Nnauye akiwa hajajulikana, Mei 15 tukio kama hilo lilitokea Masaki ambako polisi alifyatua risasi angani kumtishia aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Mkurunga, Adam Malima kwa kinachodaiwa ni kutotii amri ya Polisi.

Wakizungumza jana na JAMBOLEO kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema ni vema hali hiyo ikaangaliwa kwa jicho la ziada, huku wakitaja sababu za matukio hayo.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama alitaja sababu ya hali hiyo kuwa ni kukosekana kwa utawala wa sheria hali ambayo inaweza kusababisha hatari kwa nchi.

Alisema matukio ya kutumia silaha ilianza enzi za Mwalimu Julius Nyerere lakini alikuwa akipewa nguvu ya kisheria, kwani hakukuwa na Sheria ya Haki za Binadamu.

Lwaitama alisema wakati huu matukio hayo yakitokea ni lazima wananchi na jamii kwa ujumla wahoji, kwa kuwa wanavunja sharia, hivyo kuitaka Serikali na chama tawala kuondoa sheria zilizopo, ili kufanya wanayoyataka.

“Matukio haya yamekuwa yakitokea kipindi kirefu, ila sheria iliruhusu lakini katika Serikali ya Awamu ya Nne matukio hayo yalirudia, kwa kutekwa na kuteswa kwa Dk Stephen Ulimboka na kuuawa kwa mwanahabari Daud Mwangosi,” alisema.

Alisema matukio hayo yanaashiria kuwa CCM inaanza kuona dalili za kupotea kisiasa, hivyo kujenga taswira ya kuogopwa ili ichaguliwe tena.

Dk Lwaitama alisema utawala wa CCM unaweza kuonekana mzuri kama sheria itafuatwa, lakini kinyume chake ni kujenga mpasuko ndani ya Serikali.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala alisema sababu kubwa ya matukio hayo, ni kukosekana kwa uchumi imara unaogusa wananchi, hali ambayo inakosesha amani.

Alisema asilimia kubwa ya vijana wana msongo wa mawazo, kwa kukata tamaa kutokana na kukosa ajira, hivyo inaweza kuwasukuma kufanya matukio ambayo ni kinyume na sheria.

“Nchi yoyote pengo kati ya walionacho na wasionacho likiongezeka, litasababishia wananchi msongo wa mawazo ambao ni rahisi kuzaa matukio  ya uhalifu,” alisema.

Profesa Mpangala alisema matukio ya Pwani yanahitaji uchunguzi wa kina  wa Mamlaka husika ili kupata ufumbuzi, kwani si jambo lililozoeleka   na kuhoji sababu ya kuuawa raia tena viongozi.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe alisema anachokiona ni wananchi kuuchoka uongozi na kushindwa kuvumilia uonevu na udhalilishaji.

“Lazima tujiulize maswali mengi na si kutumia ubabe kama njia ya kutatua tatizo kwani wananchi wamechoka, hali inayowasukuma kufanya yanayotokea, wanakosa uvumilivu,” alisema.

Rungwe alisema yanayotokea ni ishara mbaya kwa nchi inayodhamira kupiga hatua ya kufikia uchumi wa kati, kwani ili kufikia hapo ni lazima wananchi washiriki kwa moyo mmoja.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda alisema anachokiona ni mfumo wa uongozi kushindwa kufuata misingi ya uongozi na kufikiria misingi isiyo sahihi.

“Mimi naona mfumo hauna ajenda, hivyo kujikuta unakuja na ajenda za matukio, ambazo hazigusi maisha ya wananchi, nadhani tunapaswa kuendesha nchi kwa ajenda rasmi,” alisema.

Danda alisema hali ya kufikia hata viongozi kutishiwa silaha wakiwa bila silaha, si ishara nzuri na kuwa siku ikitokea wasioridhika kuwa wengi, hali itakuwa mbaya zaidi.

Akizungumza hali hiyo, askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni Mohamed Ligora, alisema kinachoondelea sasa si utamaduni wa Tanzania, hivyo kupaswa kujitathmini upya.

Ligora alisema kimsingi yanayotokea yanaweza kuwa na msukumo kutoka nje, hivyo kuwataka Watanzania kutoupa nafasi msukumo huo.

“Nadiriki kusema haya yanayotokea sasa si utamaduni wetu na haikubaliki ila naona kama vile kuna msukumo wa nje wa maadui ambao hawapendi jitihada za Rais John Magufuli ambaye ameonesha nia ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kati,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo