Serikali: Jihadharini na Ebola


*Yaingia DRC, yaua watu watatu, sita wagonjwa

*Mipango ya kukabiliana nao yaandaliwa Temeke

Hussein Ndubikile

Dk. Mpoki Ulisubisya
SERIKALI imetoa hadhari kwa mikoa inayopakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuzuka kwa ugonjwa Ebola huku watu watatu wakipoteza maisha.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza Mei 12 kuwapo mlipuko wa ugonjwa huo kupitia vipimo vya maabara baada ya kugundulika wagonjwa tisa, kati yao watatu wakifariki dunia huku wengine sita wakiendelea na matibabu katika kituo kilichoandaliwa maalumu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya, alisema ugonjwa huo ulizuka katika jimbo la Kaskazini Mashariki la Bas Uele huku akisisitiza kuwa hadi sasa nchini hakuna mgonjwa aliyehisiwa kuwa na virusi vya Ebola.

“Nchi yetu inapakana na DRC, hivyo iko hatarini kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na mwingiliano wa watu hasa wanaotoka na kuingia nchini, hadhari lazima ichukuliwe,” alisema Dk Ulisubisya.

Alisema wananchi wanaoishi mikoa ya mipakani na nchi hiyo ikiwamo Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe, kuchukua hadhari na kushirikiana na Serikali ili ugonjwa huo usilete madhara.

Alisisitiza kuwa baada ya taarifa hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali zikiwamo za utoaji mafunzo kwa watumishi ya jinsi ya kuutambua na kuandaa mipangokazi ya kukabiliana nao.

Pia kupeleka vifaa kinga kwenye kituo cha Temeke kwa wagonjwa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ili kuziwezesha maabara za Taifa kutambua ugonjwa huo.

Nyingine ni utoaji taarifa ya hadhari kupitia makatibu tawala na waganga wakuu wote wa mikoa, uitishaji wa mikutano ya dharura wa uratibu wa kikosikazi cha Taifa, uundaji timu ya haraka itakayokwenda mikoa jirani na nchi hiyo na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji kwenye vituo vya mipakani vikiwamo viwanja vya ndege na bandari kavu, kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

Aidha, alisema hadhari ya ugonjwa huo haitaishia katika mikoa hiyo bali hata viwanja vikubwa vya ndege kikiwamo cha Mwalimu Julius Nyerere.

Aliongeza kuwa Ebola huambukizwa kwa njia ya kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa, kugusa maiti, kugusa wanyama wazima na walioambukizwa.

Alifafanua kuwa dalili za ugonjwa huo huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukiza baada ya siku mbili hadi 21 tangu kupata maambukizi, homa ya ghafla, kulegea kwa mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa, vidonda kooni, kutokwa damu ndani na nje ya mwili.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo