Wananchi kupewa elimu kuhusu Polisi


Suleiman Msuya

JUKWAA la Haki na Usalama limeainisha mambo 101 ambayo mwananchi anapaswa kuyajua kuhusu Polisi, huku ikitangaza mpango wa kugawa vitabu 7,000 vilivyobeba ujumbe huo, ambapo 300 kati yao vitaelekezwa kwa watu wenye mahitaji maalumu.

Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Madeline Kimei wakati akizindua na kukabidhi vitabu 20 vya nukta nundu kwa shule ya msingi ya Uhuru Mchanganyiko, Ilala Dar es Salaam jana, alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni uhuru wa majadiliano, uwajibikaji na mipaka ya kazi ya Jeshi hilo.

Alisema TLS imejipanga kugawa vitabu hivyo vitakavyosaidia jamii ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ikutanapo na polisi.

Kimei alisema TLS kwa kushirikiana na Jukwaa la Haki na Usalama imeandaa machapisho manne kuhusu polisi, mawili ni nyaraka za majadiliano kuhusu uhuru wa kioperesheni na uwajibikaji wa Jeshi hilo.

Alisema mengine mawili ni vitabu vya uelewa kwa wananchi juu ya polisi na mabaraza ya usalama ya wilaya, ambapo mwitikio umekuwa mkubwa.

“Leo tuko hapa kuzindua toleo la nuktanundu la mojawapo ya vitabu vilivyochapishwa chini ya mradi huu, na kitabu hiki kinaitwa ‘Mambo 101 Unayohitaji Kufahamu Juu ya Polisi Lakini Unaogopa Kuuliza’,” alisema.

Mjumbe huyo alisema uandaaji wa vitabu vya nuktanundu una gharama kubwa, lakini kutokana na kutambua umuhimu wa kundi hilo, walilazimika kuchapisha vitabu 300 kwa kuanzia katika kundi hilo.

Alisema lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanatambua kazi za Polisi zinavyofanywa na changamoto wanazokutana nazo.

Kimei alisema kitabu hicho kitaelimisha jamii jinsi Jeshi hilo linavyofanya kazi na ukomo wake wa madaraka, hivyo kila pande kutekeleza majukumu yake kwa haki.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Ofisa Elimu Maalumu wa Wilaya ya Ilala, Salehe Msechu alisema uamuzi wa Jukwaa la Haki na Usalama ni wa kuungwa mkono na jamii, huku akisisitiza wadau wengine kujitokeza kusaidia.

Msechu alisema Serikali imejipanga kusaidia kundi la watu wenye mahitaji maalumu, hivyo itajitahidi kutoa vifaa vitakavyotumika kwa wanafunzi wa wilaya hiyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mchanganyiko, Anna Msechu alisema shule hiyo ina wanafunzi 69 wasioona hivyo vitabu hivyo vya nuktanundu vitasaidia kutatua tatizo.

“Hapa nina wanafunzi 69 watakaofaidika na vitabu hivi; havikidhi mahitaji lakini vitasaidia kwa kiasi fulani, tunaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wasioona Tanzania, Jonas Lubago alisema vitabu vya watu wa elimu maalumu hasa wasioona nchini vinapatikana kwa chini ya asilimia moja, hivyo jitihada zinahitajika kukidhi mahitaji.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo