‘Pedeshee Ndama’ akiri tena kutakatisha fedha


Grace Gurisha

MFANYABIASHARA wa Dar es Salaam, Hussein Ndama ‘Pedeshee Ndama Mtoto wa Ng’ombe (44), amekiri mahakamani kwa mara ya pili kutakatisha fedha haramu dola 540,390 sawa na Sh bilioni 1.1.

Ndama alikiri jana mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya kusomewa mashitaka upya kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali, baada ya kukiri kosa hilo.

Kabla ya kusomewa maelezo hayo, alikumbushwa mashitaka yake saba yanayomkabili, likiwamo la kutakatisha fedha, ambapo alikiri kwa mara nyingine, huku akikana matano ya kughushi nyaraka na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya hapo, Wakili wake Jeremiah Mtobesya aliiomba Mahakama impe siku moja ya kuwasiliana na mteja wake ili kupitia maelezo hayo kabla ya kuyajibu, kwa sababu kisheria atatakiwa ayajibu mwenyewe mahakamani.

Hakimu Nongwa hakuwa na pingamizi na kuahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali, na kama mshitakiwa ataendelea kukiri kosa hilo, hukumu yake itatolewa.

Ndama alikana tuhuma za kughushi ambazo ni nne na kujipatia dola hizo kwa njia ya udanganyifu.

Hatua hiyo aliyofikia Ndama inampa mwanya wa kupata dhamana kama atalipa faini ya kiasi hicho, ambacho kinaanzia Sh milioni 100 hadi Sh milioni 500.
Ilidaiwa kuwa Februari 20, 2014 akiwa Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya, alighushi hati ya uongo ya kuuza madini nje na sampuli ya madini kwa kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Ltd imemruhusu kusafirisha makasha manne ya dhahabu ya kilo 207 na thamani ya dola 8,280,000 sawa na zaidi ya Sh bilioni 16 huku akijua si kweli.

Katika tuhuma za pili, mshitakiwa anadaiwa kuwa Machi 6, 2014  akiwa Dar es Salaam alighushi hati inayotoka ofisi za Umoja wa Mataifa, Dar es Salaam kwa kuonesha kuwa kilo 207 za dhahabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilitarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru kwenda kampuni  ya Trade TJL DTYL Ltd ya Australia na kwamba hazikuwa na jinai yoyote.

Ilidaiwa kuwa Februari 20, 2014 alighushi nyaraka za malipo namba R. 28092 ya Februari 20, 2014 kwa kuonesha kuwa Muru ililipa kodi ya dola 331,200 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuingiza kilo 207 za dhahabu zenye thamani ya dola 8,280,000 zilizokuwa zikitoka DR Congo huku akijua si kweli.

Ndama anadaiwa pia kuwa Februari 20, 2014 alighushi bima kutoka kampuni ya Phoenix of Tanzania Assurance Ltd ya tarehe hiyo kuonesha kuwa Muru iliyawekea bima makasha manne ya dhahabu huku akijua si kweli.

Akiendelea kusoma hati ya mashitaka, Msigwa alidai kuwa Ndama kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014 akiwa Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya, alijipatia dola 540,390 kutoka Trade TJL DTYL Ltd kwa maelezo kuwa ataipa na kusafirisha kilo 207 za dhahabu.

Katika tuhuma za sita, Ndama anadaiwa kuwa  kati Februari 26 na Machi 2014 akiwa Dar es Salaam, alijihusisha na muamala wa dola 540,390 huku akijua ni za uhalifu kwa kuelekeza fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti namba 9120000085152 ya benki ya Stanbic kwa jina la Muru na baada ya fedha hizo kuingizwa, mshitakiwa alizitoa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo