Profesa Mukandala awafunda wahitimu Kidato cha Sita


Mwandishi Wetu

Profesa Rwekaza Mukandala
​MAKAMU Mkuu  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Rwekaza Mukandala, amewataka vijana wanaohitimu kidato cha sita nchini kuwa makini na wasikubali kusombwa na ‘mawimbi’ ya dunia.

Akizungumza katika Mahafali ya Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya St Joseph Cathedral, Profesa Mukandala mbali na kuwapongeza wahitimu 237 alisema, “Kwa hatua mliyofikia kila mmoja anapaswa atafakari kwa kina wito wake kimaisha. Kuweni makini, msisukumwe na mawimbi ya dunia na kujikuta mmepoteza ndoto zenu.”

Profesa Mukandala aliendelea “Kuhitimu kidato cha sita si jambo dogo. Ni hatua ya kuwaongoza kujiandaa na utu uzima, ikiwemo kujiunga na elimu ya vyuo vya elimu ya juu na kuingia kwenye ndoa. Ni muda wa kutathmini yale uliyopitia na kutafakari maisha yako ya baadaye. Ni fursa ya kutoa shukrani kwa Mungu, kwa wazazi na walimu ambao walifanya kazi kwa umakini na kujitoa ili mfikie hatua nzuri mliyopo sasa.”

“Mnapaswa kuepuka mwenendo wa kujiona wanyonge, au mtu asiyeweza kutimiza ndoto zake. Jenga tabia ya kuwa makini na maisha yako, jali mazingira yako na maendeleo yako,” alisisitiza.

Aliwataka wahakikishe wanakuchukua hatua mahsusi na kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma wanazozitaka.

Aliwataka wawe waadilifu na wenye heshima kwa watu wote, pia akawaasa juu ya maisha ya kutaka kupata fedha kwa haraka na kujilimbikizia mali.

“Epukeni rushwa na ufisadi. Mnatakiwa kujua kuwa utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa fedha ingawa nayo ni muhimu katika maisha. Msitegemee kuishi kwa kuzingatia mambo makubwa yanayopimika kwa fedha,” alisema.

Akitoa mfano, Prof. Mukandala alisema: “Msikimbilie kuwa na magari mengi bila kujua nani atayatumia, au kujenga nyumba kubwa bila kujua nani atahitaji nafasi hiyo kubwa. Unanunua simu mbili au tatu bila kufikiria athari zake kwa afya na mahusiano yako. Kabla hujachukua hatua ni lazima ujiulize, je unakihitaji kitu hicho? Kuweni makini na matumizi ya fedha badala kujilimbikiza vitu vya anasa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo