Majaliwa ataka matangazo sekta ya Utalii


Mwandishi Wetu

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka maofisa wanaosimamia sekta ya utalii nchini kuitangaza kwa nguvu ili kuvutia watalii wengi zaidi.

Akizungumza katika mkutano wa 10 wa Baraza la Taifa la Biashara, Ikulu jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Majaliwa alisema kuna fedha nyingi serikali inazikosa katika utalii kwa kushindwa kutangaza vivutio vyake.

“Sekta binafsi ndiyo itakayotupa mwelekeo wa uchumi wetu hatuna budi kutilia nguvu mambo muhimu, kama kuna tatizo liletwe katika meza ya majadiliano tujue namna ya kulitatua,” alisema.

Alisema Tanzania bado iko nyuma kwenye utalii na maeneo mengi ya wazi hatuyatumiki kuweka matangazo.

“Ukienda viwanja vya michezo hakuna matangazo, barabara hizi kuanzia mwanzo hadi mwisho yamejaa matangazo ya kampuni za simu pekee, ukishuka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere hukuti tangazo lolote la utalii. Kuanzia leo natoa agizo taasisi zote za utalii zitangaze vivutio vyake. Mbuga zetu zina vivutio vingi vitangazeni tena mtangaze vizuri sio mnajitangaza bila kufuata mpangilio,” alisema Majaliwa.

Awali baadhi ya wajumbe waalikwa kwenye mkutano huo walipopata fursa ya kuzungumzia changamoto wanazokumbana nazo kwenye sekta ya utalii walisema kikubwa ni kutoshirikishwa kwenye uundwaji wa sera hasa suala la tozo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mkurugenzi wa Kibo Guides, kampuni inayojishughulisha na kutembeza watalii na hoteli jijini Arusha, Willy Chambulo alisema:

“Sekta binafsi inajitahidi kuliletea Taifa mapato lakini hatupati mrejesho mzuri.”

Akitoa ushauri alisema: “Kuwepo mawasiliano ya mara kwa mara kati ya taasisi za Serikali na wafanyabiashara, suala hili ni letu sote na tunafurahi tunapoiingizia mapato Serikali yetu lakini tuelezwe hata mwaka mmoja kabla ili tujipange.”

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema ni lazima kodi ilipwe ili kulinda mazingira katika maeneo ya utalii na wanyama kupata huduma ikiwemo ulinzi na matibabu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo