Nilisikia Gwajima amefariki, mchungji aieleza Mahakama


Grace Gurisha

Askofu Gwajima
MCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, George Milulu, ameieleza mahakama kuwa alisikia uvumi kwamba Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Josephat Gwajima (47) amefariki dunia katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.

Milulu aliyaeleza hayo juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala kutoa utetezi wake katika kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi inayomkabili Askofu Gwajima.

Alidai kuwa Machi 29, 2015 alikuwa hospitali ya TMJ, ambapo alikwenda baada ya kupata taarifa ya uvumi kwamba Askofu Gwajima amekufa.

Alieleza kuwa alipofika hospitalini alikuta watu ni wengi, lakini muda mfupi baadaye waliamuliwa na polisi wakae eneo moja ikiwamo waliokuwa waumini waliokuwa juu ya ghorofa ambapo waliamriwa washuke chini.

Mchungaji huyo alidai licha ya kutoambiwa sababu ya kutakiwa wakusanyike eneno moja, ilitolewa amri nyingine ya kuwqataka waingie ndani ya gari la polisi aina ya Land cruiser na kupelekwa kituo cha polisi Oysterbay.

Alieleza kuwa walipofika kituoni hapo waliamriwa wavue mikanda, viatu na kuingizwa rumande ambapo wakaanza kutolewa mmoja mmoja na kuhojiwa. Hata hivyo, alikataa kuliona begi ambalo lilikuwa na vitu mbalimbali vya Gwajima ikiwamo bastola.

Naye, shahidi George Mzava alieleza kuwa hajawahi kukutwa na begi lolote katika hospitali ya TMJ kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka. Alidai baada ya kukamatwa na polisi walifikishwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambapo waliamriwa wavue mikanda na kuanza kuhojiwa mmoja mmoja.

Alipoulizwa na Kibatala kwamba anazijua sababu za kuingizwa mahabusu, alieleza kuwa hawakuambia sababu na walikuwa wakiandika maelezo kwa shinikizo.

Katika kesi hiyo, mbali ya Askofu Gwajima washtakiwa wengine ni George Mzava, Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze (39) na Georgey Milulu wao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki Bastola aina ya Berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha sheria.

Wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A walikutwa wakimiliki bastola aina ya berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo