RC awatoa hofu wafanyakazi waliokuwa CDA


Suleiman Msuya

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amewatoa hofu wafanyakazi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na wananchi wa Manispaa hiyo kuhusu stahiki zao.

Amebainisha kuwa Serikali imeunda tume ya kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa baada ya kuivunja Mamlaka hiyo.

Kauli hiyo ya Rugimbana imekuja siku moja baada ya baadhi ya wananchi wa Manispaa hiyo, kuonekana katika ofisi za CDA wakitaka kujua hatima ya viwanja na michoro waliyoomba kwa Mamlaka hiyo.

Alisema tume hiyo itahusisha Mamlaka ya Utumishi wa Umma, ambayo itahusika na kuhamishia watumishi kwenye sekta mbalimbali kama ardhi, serikali za mitaa na Manispaa yenyewe.

Mkuu huyo alisema pia tume itaangalia utaratibu wa kuhamisha nyaraka ambapo ofisi ya Waziri Mkuu imechukua jukumu kwa kushirikisha TAMISEMI ambayo inaunda tume husika na mkoa husika kupitia Katibu Tawala wa Mkoa.

“Kwa sasa kinachofanyika ni mamlaka zinazohusika kutafsiri agizo la Rais kivitendo, kuhakikisha watumishi wote wanasambazwa katika ofisi mbalimbali na pia kuhakikisha wanapata haki zao,” alisema.

Alisema hakuna sababu ya wafanyakazi kufikiria maslahi kwa sasa, kwani ndio mchakato umeanza huku akisisitiza kuwa watumishi wote watapata kazi kwenye sekta mbalimbali.

Kuhusu wananchi kupata hati au ramani, alisema hakuna mwananchi aliye na hati halali ya CDA atakayepewa nyingine kwa mfumo wa Mamlaka itakayokuwapo.

“Kamati hii inashirikisha sehemu mbalimbali, hivyo wananchi na wafanyakazi wawe na Amani, ila sasa huduma za CDA zimesitishwa kwa muda ili kukamilisha mchakato wa kukabidhi nyaraka husika,” alisema. 

Akizungumza baada ya utiaji saini Amri ya Rais, Rais Magufuli alisema ameivunja CDA na kuhamishia majukumu yake kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji huduma kwa wananchi uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya CDA.

Magufuli pia aliivunja Bodi ya CDA, na kusema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine na kuagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi zingine za Serikali kadri inavyofaa.

Aidha, aliagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33 zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini, ili kuvutia wawekezaji hasa wa viwanda.

CDA ilianzishwa kwa Amri ya Rais Aprili mosi 1973 na kutangazwa kupitia Tangazo la Serikali namba 230 na ilivunjwa rasmi Mei 15 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo