Airtel yaingia ubia na redio za jamii


Suleiman Msuya

KAMPUNI ya Simu ya Airtel na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (Unesco) wameazimia kushirikiana kuinua uchumi na kuboresha elimu kwa kutumia redio za kijamii.

Meneja wa Huduma za Jamii wa kampuni hiyo, Hawa Bayumi alisema kuwa ushirikiano huo utazifanya redio hizo kutumia minara ya Airtel kurusha matangazo yake, kutoa huduma za intaneti na huduma za fedha.

Bayumi alibainisha kuwa ushirikiano huo utazihusisha redio tisa za maeneo mbalimbali nchini.

Alizitaja redio zitakazonufaika kuwa ni Radio Fadeco ya Kagera, Kyela FM (Mbeya), Pangani FM (Tanga), Kahama FM (Shinyanga), Uvinza Radio (Kigoma), Sengerema Radio (Mwanza) na Loliondo Radio ya Arusha huku Mtegani FM ya Zanzibar na Micheweni ya Pemba zikiwa bado hazijajihusisha na mpango huo kikamilifu.

“Mpaka sasa ushirikiano huu ushafikia jumla ya redio saba na kwa kutumia minara ya Airtel ambayo iko kwenye maeneo yao, redio hizi zimeweza kuboresha ubora wa matangazo na kufikia maeneo mengi na wasikilizaji wengi, alisema Bayumi,” alisema.

Katika kuboresha elimu pamoja na kuinua hali ya kiuchumi, Meneja Miradi UNESCO, Nancy Kaizilege alisema shirika hilo linasaidia redio za kijamii kwa kuwajengea uwezo watangazaji pamoja na waandaji wa vipindi kwa huduma bora na pia kuweka mkazo kwenye elimu ya haki za kibinadamu.

Alisema wamekuwa wakisisitiza habari zinazohusu watu wenye ulemavu wa ngozi, changamoto za uzazi na elimu ya uzazi wa mpango, elimu kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na kumwezesha mtoto wa kike.

Kaizilege alisema pia vipindi vyenye kujadili heshima ya mwanamke kwenye jamii jambo ambapo kwa kiasi kikubwa limesaidia kupunguza ndoa za utotoni.

“Tumeshuhudia siku za karibuni radio hizi zikileta wadau mbalimbali pamoja na kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo kwa mfano wilaya ya Kahama imeweza kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara kwa kushirikiana na migodi ya uchimbaji madini,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo