Mambo 10 yamweka JPM mtegoni


*Wasomi wadai vilio vya wananchi vimeongezeka

Waandishi Wetu

Rais John Magufuli
SERIKALI ya Awamu ya Tano imefanya vizuri tangu ilipoingia madarakani, ikifanikiwa pamoja na mambo mengine kurejesha nidhamu ya kazi na kuwajibisha viongozi na watumishi wa umma.

Aidha, imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwamo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, ununuzi wa ndege, kuzuia matumizi yasiyo ya lazima na kufuta maadhimisho ya sherehe mbalilimbali ni baadhi ya mambo yaliyofurahiwa na wengi.

Hata hivyo, wakati Serikali hiyo inayoongozwa na Rais John Magufuli ikikaribia kumaliza mwaka wa pili, baadhi ya wasomi na wanasiasa wametaja mambo 10 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kutokana na utekelezaji wake kuathiri kundi kubwa la Watanzania wakisema yanaweza kumweka mtegoni.

Wamesema licha ya kuwa baadhi ya mambo hayo yamefanyika kwa nia njema, utekelezaji wake ulikuwa na kasoro, huku wakikosoa baadhi ya kauli, hatua sambamba na kufanyika mambo waliyosema hayana ulazima kwa sasa.

“Matukio hayo yana maana kubwa sana kwani wananchi wamejawa na hasira hakika wanahifadhi hasira zao kuelekea mwaka 2020,”alisema Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini.

Mambo kumi yanayomweka JPM mtegoni

Mikutano ya hadhara
Marufuku ya mikutano ya siasa mpaka wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 kama ilivyotangazwa na Rais Magufuli ni moja kati ya uamuzi ulioathiri wanasiasa na vyama, hasa vya upinzani.

Sababu iliyotolewa na Rais Magufuli ni kuwa huu ni muda wa kufanya kazi na siyo siasa. Katika kufafanua kauli yake, Rais alisema wabunge na madiwani tu ndiyo wanaoruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo yao na hawaruhusiwi kuleta wageni kutoka nje.

2. Bomoabomoa
Mwanzoni mwa utawala wake liliibuka zoezi la kuondoa watu waliojenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Bomoabomoa hiyo iliendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuathiriwi watu wengi masikini ambao ndiyo waliomchagua pia Rais huyo wa Awamu ya Tano.
Zoezi hilo lililenga nyumba zilizojengwa mabondeni, kwenye fukwe za bahari ya Hindi, kingo za mito na maeneo ya wazi na hivi karibuni wamebomolewa waliojenga pembezoni mwa reli ya kati.

3. Matangazo ya Bunge ‘live’
Kusitishwa kwa urushwaji wa matangazo ya Bunge moja kwa moja nao umewagusa baadhi ya wananchi ambao tangu kutolewa katazo hilo wamekuwa wakilipinga licha ya kuwa baadhi ya televisheni hurekodi na kurusha usiku.

Machi mwaka huu chombo kimoja cha habari kiliandika kuwa Rais Magufuli katika kikao chake cha ndani na wabunge wa CCM mjini Dodoma, aliwaeleza kuwa yeye ndiye aliyeamua kusitisha mikutano ya Bunge kuoneshwa moja kwa moja katika televisheni.

4. Wabunge wa CCM kutowatembelea wa upinzani
Katika kikao hicho pia iliripotiwa jinsi Rais Magufuli alivyoshangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda kumtembea mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alipokuwa gerezani jambo alilolifananisha na usaliti kwa chama chake.
Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili. Kauli hiyo ambayo haijakanushwa popote ilizuia taharuki huku wasomi waliotoa maoni katika gazeti hili wakitofautiana mtazamo wao.

5. Utumbuaji majipu
Baada ya kuapishwa Novemba 5, mwaka 2015 Rais Magufuli alianza utekelezaji wa majukumu yake kwa mfumo wa kuwajibisha watendaji wazembe, wala rushwa na wanaolisababishia Taifa hasara kwa njia mbalimbali. Mfumo huo wa utendaji kazi umejipatia umaarufu kuwa ‘utumbuaji majipu’.
Licha ya utumbuaji huo kuungwa mkono, wapo walioukosoa wakitaka watakaotumbuliwa wawe watu waliobainika kuwa na makosa na kasoro mbalimbali, ukiwakumbe hadi watumishi wasiohusika.
Tangu kuanza kwa utumbuaji, zaidi ya watumishi 1,000 wameshatumbuliwa jambo linalowafanya katika maisha yao kutosahau utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

6. Kufuta safari za nje
Uamuzi wa Rais kubana matumizi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti ziara za nje zisizo na tija, safari za mafunzo nje ya nchi, warsha, semina, makongamano na matamasha ulisifiwa na kada mbalimbali nchini lakini kwa kiasi fulani uliacha simanzi kwa watumishi, hasa waliokuwa wakitumia maeneo hayo kujipatia fedha za bure.

7. Pesa kutoweka, kupunguzwa kazi
Wapo wanaofurahia hatua za Serikali kuthibiti na kubana matumizi, lakini uamuzi huo umeathiri sekta nyingi kutokana na fedha kutoweka.
Si hoteli, baa, mashirika ya usafiri, kampuni za huduma za chakula, vyombo vya habari wala viwanda zilizoepuka athari za uamuzi huo wa Serikali.
Katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano, ulioshuhudia fedha kutoweka baadhi ya mashirika na taasisi hasa binafsi zililazimika kupunguza wafanyakazi wake, huku baadhi ya wafanyabiashara wakifunga biashara kutokana na mzunguko wa fedha kuwa hafifu wakilazimika kufanya hivyo ili kwenda sambamba na uzalishaji na kupata faida.

8. Vyeti feki
Uhakiki wa vyeti unaofanywa na Serikali kwa kiasi kikubwa umeacha alama nyingine kwa Watanzania. Baada ya kupokea majina 9,932 kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Umma na Utawala Bora), Rais Magufuli aliagiza wote waliotajwa kughushi vyeti waondoke vituo vya kazi kabla ya Mei 15 na watakaokaidi watafikishwa mahakamani.
Pengine sio ajabu kutajwa kwenye orodha hiyo kwa kuwa ukaguzi haukuacha mtu au cheo, lakini kugundulika kwake kunaibua maswali zaidi katika uhakiki huo ambao tayari uemshaonyesha dosari kama kutaja majina ya baadhi kuwa wana vyeti vya kughushi vya elimu ya sekondari wakati hawakuviwasilisha kwenye uhakiki uliofanyika.

9. Tetemeko la ardhi Kagera
Septemba 11 mwaka jana mikoa ya kanda ya ziwa ilikumbwa na tetemeko la ardhi ambako watu takribani 17 walipoteza maisha, huku zaidi ya nyumba 840 zikibomona na nyingine 1,264 kuharibika.
Wakati akipokea taarifa ya maafa hayo, Rais Magufuli alisema Serikali itarekebisha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na kuwataka waliobomolewa nyumba, wajipange kuzirekebisha.
Serikali ilizuia watu au taasisi kutoa misaada kwa waathirika, badala yake ikaagiza wapiti Ofisi ya Mkuu wa Mkoa  huku kipaumbele kikiwa ni kukarabati miundombinu jambo ambalo lilipingwa na kulalamikiwa na watu waliotaka fedha hizo ziende moja kwa moja kwa waathirika.

10. Kudhibiti mihimili
Licha ya Seriklai kuwa na wajibu wa kutafuta fedha, kitendo cha Mahakama na Bunge kuwa mihimili inayojitegemea lakini kujikuta ikipangiwa mambo kadha wa kadha na Serikali kumezungumziwa na wachambuzi wa masuala mbalimbali nchini kuwa si utaratibu mzuri.

Mfano ni uamuzi wa Rais kuagiza fedha za sherehe ya kuwapongeza wabunge kutumika kununulia vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Maoni ya wasomi, wanasiasa

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari alisema suala la kuzuia mikutano ya hadhara na kutokuonesha Bunge ni moja ya mambo ambayo yanaweza kumnyima Rais Magufuli nafasi ya kutetea kiti chake.

“Rais anasema hakuna siasa na wananchi wafanye kazi lakini anashindwa kuelewa kwamba kuwaminya huko na kuwatengenezea watu hofu ya kushindwa kuzungumza kunawafanya wazidi kuwa majasiri na siku wakipata nafasi ya kufanya maamuzi katika chumba cha kura basi hawatomchagua,”alisema.

“Uhusiano wake na wananchi umedorora kwa kuwa anawafanya wawe kimya na hofu lakini akae akijua kuwa 2020 watu wataikimbia minyororo kwa kuwa anasema analeta maendeleo lakini utekelezaji hakuna na watu wakijaribu kumkosoa wanatishwa na kukamatwa.”

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema inawezekana Rais akabadilika baadayee kwa kuwa kisiasa bado miaka ni mingi kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Mbunda alisema mbali na mambo hayo, suala la ukata kwa wananchi walio wengi ndio limegeuka ajenda huku akitolea mfano jinsi anavyozungumzia hovyo katika mitandao ya kijamii.

“Nadhani demokrasia inawapa nguvu  wananchi kuliko viongozi kwa kuwa wao ndio wanaochagua lakini hapa kwetu viongozi walio wengi huwa wanyenyekevu pindi wanapoomba kura lakini wakishapata madaraka huwasahau wapiga kura wao,”alisema.

“Kuna mambo mengi yanaweza kukwamisha safari yake 2020 mfano suala la kuonekana kutojali wananchi wake ukirejea kauli yake wakati wananchi wakilalamika njaa, chakula hakuna yeye akawaambia Serikali haitoi chakula hiyo maana yake Serikali haijali.”

Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk Onesmo Kyauke alikuwa na mtazamo tofauti kuwa mambo hayo hayawezi kuwa sababu ya Rais Magufuli kurudi madarakani lakini akaonya kuwa anapaswa kubadilika ili kurudisha imani ya wananchi waliyokuwa wamejenga kwake.

“Mfano suala la Bunge Live ni haki ya Wananchi karibu nchi zote duniani wanonesha Bunge, ni jambo la hatari kuwanyima watu haki zao za msingi, hata kama Sheria haisemi lioneshwe lakini Sheria hiyo hiyo haikatazi Bunge Live,”Alisema Dk Kyauke.

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alitaja uamuzi wa kufuta mikutako ya hadhara, kubainisha kuwa jambo hilo litampa wakati mgumu Rais Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.

“Pia kuzuia mikutano ya Bunge ni dosari kubwa kwake, katika utawala wake kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, kukandamiza demokrasia na kutunga sheria kandamizi,”alisema Kafulila na kubainisha suala la vyeti feki ni sahihi kufanyika.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo