Meya Dar aahidi kupunguza deni la uzio


Suleiman Msuya

Isaya Mwita
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, ameahidi kusaidia kupunguza deni la Sh milioni 16 linalodaiwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Ushirombo kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa makaburi ya Tambaza.

Alisema hayo jana wakati wa dua maalumu ya kumwombea marehemu Shekhe Yahya Hussein sambamba na kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Mwita alisema kwa nafasi yake atajitahidi kusaidia kupunguza deni hilo kama si kulimaliza kabisa kutokana na umuhimu wa watu waliopumzishwa katika eneo hilo.

Alisema hafanyi jambo hilo kisiasa ama kufurahisha Waislamu, bali ni kutokana na kutambua umuhimu wa watu waliolala eneo hilo.

“Nimesikia kwenye risala yenu, kuwa mna deni la ujenzi wa uzio wa makaburi, sitasema nitachangia kiasi gani, ila nitapunguza kwa nafasi yangu kiasi ambacho mnadaiwa,” alisema.

“Watu ambao leo hii tunawakumbuka wamelala hapa, walikuwa na mchango mkubwa, kila mmoja anatambua hilo, waliitangaza nchi yetu kwenye mambo ya dini na ya kimaendeleo,” aliongeza.

Aidha, Mwita aliwasihi waumini wa dini ya kiisilamu, katika kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wajikite katika kuendeleza mambo mema.

Alisema ufike wakati kila muumini, kutambua umuhimu wa kutenda na kuendeleza mema aliyofanya wakati wa Mfungo, kwani kufanya hivyo kutamweka kwenye nafasi nzuri kiimani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo