Bosi Halotel, wenzake watozwa milioni 700/-


Grace Gurisha

Do Many Hong
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Halotel Viettel Tanzania Ltd, Do Many Hong na wenzake saba kulipa zaidi ya Sh milioni 700, baada ya washitakiwa hao kukiri kutenda makosa saba kinyume na taratibu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Pia imewaamuru washitakiwa hao kuirudishia TCRA, Sh milioni 459, baada ya kukiri kuisababishia hasara hiyo, kutokana na kufanya biashara hiyo ikiwamo kufunga vifaa vya mawasiliano bila kufuata utaratibu.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri, baada ya washitakiwa hao kukiri kutenda makosa hayo, ambapo alisema watatakiwa kulipa Sh milioni tano kwa kila kosa na pia vitu vya mawasiliano ambavyo walikutwa navyo vichukuliwe na Serikali.

“Kila mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh milioni tano kwa kila kosa na ile hasara mliyoisababishia Serikali muilipe TCRA na vile vitu walivyokutwa navyo vichukuliwe na Serikali,” alisema Mashauri.

Baada ya kutoa hukumu hiyo, aliwaeleza kuwa wanaweza kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, kama hawajaridhika na adhabu aliyoitoa.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Jehovanes Zacharia aliwaondolea mashitaka matatu washitakiwa hao, ambayo ni kula njama, kuwasilisha nyaraka za uongo na kughushi na kubaki saba, kwa sababu awali walikuwa wakituhumiwa kwa makosa 10.

Baada ya hapo, washitakiwa walikiri kutengeneza  mfumo wa kutumia huduma za mtandao kwa lengo la kukwepa kodi na makosa mengine sita. Walisomewa maelezo yao ya awali kuhusu tuhuma zao wakakiri tena, wakatiwa hatiani.

Hata hivyo, Zacharia alidai kuwa hawana kumbukumbu kama washitakiwa hao walitenda makosa ya jina, kwa hiyo Mahakama iwape adhabu stahiki.

Mbali na Hong, wengine ni Dilshad Ahmed (36), Rohail Yaqoob(47), Khalid Mahmood (59), Ashfaq Ahmad (38), Muhamad Aneess(48), Imtiaz Ammar (33) wote raia wa Pakistani na Ramesh Kandasamy (36) wa Sri-Lanka.

Ilidaiwa kuwa Novemba 20, mwaka jana washitakiwa waliingiza vifaa vya elektroniki bila leseni na katika siku isiyofahamika Novemba mwaka jana, walisimika vifaa hivyo ikiwamo sim box yenye namba ya siri 1152000.8.n.t.n na kompyuta mpakato mbili aina ya Dell bila kibali cha TCRA.

Katika kipindi hicho, washitakiwa hao waliunganisha vifaa hivyo na huduma za mitandao kwa lengo la kupokea na kusambaza mawasiliano bila kuthibitishwa na TCRA.

Hong ilithibitishwa kuwa kati ya Novemba mwaka jana na Februari maeneo ya ofisi za Halotel Victoria Kinondoni, alishindwa kuthibitisha taarifa iliyotolewa na Unex Company Ltd kwa lengo la kusajili simu 1,000.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo