Treni Dar-Moro yasimamishwa wiki mbili


Abraham Ntambara

KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL), imesimamisha kwa muda wa siku 14 huduma ya usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ili kupisha marekebisho ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Masoko wa TRL, Shaban Kiko alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu daraja la reli la Ruvu kutitia upande mmoja.

Kutokakana na hali hiyo, alisema abiria 257 waliotakiwa kusafiri jana kutoka Dar es Salaam, watasafirishwa leo kwa mabasi na kampuni hiyo hadi Morogoro kili kuendelea na usafiri wa treni.

“Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na kipande cha reli kati ya Dar es Salaam na Ruvu kuwa haipitiki,” alisema Kiko.

Alisema mamlaka husika zinafanyia kazi ukarabati wa daraja hilo ili njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ifunguliwe ndani ya muda mfupi iwezekanavyo.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka abiria wanaosafiri leo kufika kituo kikuu cha reli Dar es Salaam kabla ya saa moja asubuhi, ili wasafirishwe kwa mabasi maalumu yaliyokodiwa na TRL hadi Morogoro ambako watapanda treni kwenda Bara, itakayoondoka saa moja usiku.

Akizungumzia wafanyabiashara wasafirishao shehena kwenda Bara, aliwataka kuwasiliana na Idara ya Masoko ya TRL ili kupewa utaratibu wa jinsi ya kusafirisha mizigo yao hadi Morogoro ambako itapakiwa kwenye treni kwenda Bara.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TRL, Profesa John Kondoro na wajumbe wengine wa Bodi hiyo jana asubuhi walitembelea eneo la daraja hilo kufanya tathmini ili kuruhusu maandalizi ya ukarabati kuendelea.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo