Star TV kuadhibiwa kama Bashite


Mwandishi Wetu

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeionya televisheni ya Star TV kuwa itageuka adui wa tasnia ya habari, kama itaendelea na kusudio lake la kurusha mahojiano maalumu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mbali na onyo hilo, TEF pia imetangaza kumfuatilia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutokana na kuibuka kwa matukio mbalimbali ya kudhalilishwa waandishi wa habari kwa amri zake.

Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema hayo jana katika taarifa yake kwa umma, ambapo alirejea sababu za kususiwa kwa habari za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema Machi, TEF ilikubaliana kutotangaza habari za Mkuu huyo wa Mkoa, baada ya kufanya uvamizi kwenye kituo cha televisheni cha Clouds Machi 17.

Katika uvamizi huo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na askari wenye bunduki, ambao ulikuwa ni mwendelezo wa matukio ya kudhalilisha vyombo vya habari.

“Uamuzi huo ulifikiwa kwa pamoja baina ya TEF na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kuungwa mkono na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (Moat) na taasisi nyingine za kihabari nchini,” alikumbusha Balile.

Alisema Mkuu huyo wa Mkoa alionekana kudhalilisha wanahabari, kutukana na kutoheshimu taaluma ya habari.

Alifafanua kuwa baada ya uvamizi wa Clouds, TEF ilimpa masharti mepesi Mkuu wa Mkoa ya kuomba radhi waandishi wa habari, kama sehemu ya uungwana wa kitanzania, ili arejeshe uhusiano na tasnia ya habari.

Kwa kuwa hajaomba radhi, TEF ilisema uamuzi unaotaka kufanywa na kampuni ya Sahara Communications Limited wamiliki wa Star TV, kuhojiana na Mkuu huyo ni usaliti wa hali ya juu kwa taaluma ya habari, kwa kuwa imekubalika kutotangaza habari zozote zinazomhusu Mkuu huyo.

“Tulisema katika tamko hilo, kuwa yeyote atakayeshirikiana na Mkuu huyo wa Mkoa, naye tutamhesabu kama adui wa tasnia ya habari nchini.

“Kwa mantiki hiyo, tunasema ikiwa Star TV wameamua kushirikiana naye basi ni wazi wameamua kwa hiyari yao kujitangaza kuwa adui wa tasnia.

“Kila Mtanzania anajua jinsi ya kupambana na adui kwa nia ya kujilinda na tasnia haitasita kufanya hivyo,” alisema Balile.

Kuhusu Gambo, alisema TEF inafuatilia kwa karibu uhusiano wake na vyombo vya habari kutokana na matukio ya mara kwa mara ya kudhalilisha wanahabari kazini kwa amri zake.

Alionya kuwa ikiwa matukio hayo yataendelea, TEF italazimika kupitia uhusiano huo.

Alipongeza vyombo vya habari; magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii ya ndani na nje ya nchi, kutekeleza uamuzi wa kumfungia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu, licha ya ushawishi wa hapa na pale unaotolewa na wapambe wake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo