Sababu za Malima kukamatwa zaanikwa


Hussein Ndubikile na Grace Gurisha

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetaja sababu tatu za kumkamata aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, katika tukio lililombatana na kufyatua risasi tatu angani.

Mtuhumiwa huyo jana alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu tuhuma zinazomkabili na kutetewa na Wakili Peter Kibatala.

Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa mitandaoni picha za video zikionesha gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T 296 ATW, ambalo liliegeshwa pembeni karibu na hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam, wakashuka askari wawili – mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na mwingine polisi wa kawaida.

Akizungumzia suala hilo jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema tukio hilo lilitokea juzi saa sita mchana Masaki karibu na ofisi za Ubalozi wa Canada, ambapo mfanyakazi wa kampuni ya Priscane Business Enterprises, alikuta gari la Malima limeegeshwa sehemu isiyotakiwa, huku akisisitiza dereva wa gari alipotakiwa alipeleke gari hilo yadi alikaidi na kulirudisha kwa nguvu lilipokuwa.

“Mfanyakazi wa Priscane alilikuta gari la Malima likiwa na dereva aliyeambiwa ameegesha sehemu isiyoruhusiwa, lakini cha kushangaza alikaidi ndipo mvutano ukaanza kati yake na mfanyakazi huyo na kulazimu polisi kuingilia kati,” alisema Kamanda Sirro.

Katika video ya tukio hilo, askari wa FFU baada ya kushuka kwenye gari hilo alionekana akinyanyua bunduki na kufyatua risasi angani, kabla mwenzake kumfuata na kumshika kifuani na kutaka kumrudisha kwenye gari.

Tukio liliendelea kwa askari aliyemfuata mwenzake kumfuata Malima na kuzungumza naye, lakini wakati wakiendelea na mazungumzo, yule askari aliyefyatua risasi pia alimfuata na kumsukuma mara mbili waziri huyo wa zamani, kisha kuinua juu bunduki na kusikika akitamka:

“Kwa nini hamheshimu Serikali nyie, mzee heshimu Serikali, mimi nimewekwa kuitumikia Serikali, siwezi kudharaulika.”

Katika video hiyo pia ilisikika sauti ya mtu ambaye hakuonekana akitamka:  “Huna mamlaka, huna mamlaka ya kutishia.”

Wakati hayo yakiendelea, Malima alionekana kujibizana na askari hao akiwa ameweka mikono mfukoni mwa suruali yake, huku mmoja wa askari hao aliyeonekana akimsihi mwenzake aende kwenye gari akitamka: “Poti, Poti, Poti ee!”

Katika mkutano wake na wanahabari, Kamanda Sirro alisema Malima alipotoka nje ya Ubalozi huo, askari walimwambia gari lake linatakiwa liende yadi kwa sababu lilikiuka sheria za maegesho, lakini alionekana kukaidi hali iliyolamzimu askari huyo kufyatua risasi tatu angani.

Alisema licha ya amri ya askari, Malima aliendelea kukaidi huku akitamka kuwa yeye amefanya kazi na viongozi wakubwa, hali iliyomlazimu askari kufyatua risasi nyingine.

Sirro alisema: “Kelele za watu waliokuwa wakizomea, zilichangia askari kutumia busara kupiga risasi hizo angani ili kuwatawanya na endapo   wangewaacha Malima na dereva wake, ingechangia kuwaaminisha wananchi kuwa polisi wameshindwa kufanya kazi yao.”

Alitaja sababu nyingine kuwa ni mazingira hatarishi yaliyomlazimu askari huyo kufyatua risasi, kulingana na wakati na kwamba askari wangeondoka eneo la tukio bila kuwakamata, wangeshitakiwa kwa woga.

Aidha, alisema waziri huyo wa zamani alifikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili yakiwamo ya kuzuia polisi kufanya kazi zao, kujeruhi na kukaidi amri.

Mahakamani

Malima na dereva wake, Ramadhani Kingwande walipandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya kuzuia polisi kufanya kazi yake na kujeruhi.

Kesi hiyo inawakutanisha Wakili Kibatala na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono.

Wakili Mwanaamina alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage kuwa Malima ambaye alikuwa Mbunge wa Mkuranga  na dereva wake wabnakabiliwa na mashitaka mawili.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Mei 15 Masaki Kinondoni, Dar es Salaam.

Wakili huyo alidai kuwa Kingwande kwa nia ya kukataa kukamatwa kutokana na kuegesha vibaya gari lake namba T 587 DDL, alimjeruhi Mwita Joseph ambaye ni Ofisa Operesheni wa kampuni ya Priscane Business Enterprises na kumsababishia maumivu makali.

Wakili huyo alidai kuwa Malima alitenda kosa la shambulio, Mei 15     Masaki, wakati akimzuia dereva wake kukamatwa baada ya kutuhumiwa kutenda kosa  barabarani.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo, Malima alimzuia askari Polisi namba H 7818 Konstebo Abdu kufanya kazi halali ya kumkamata Kingwande aliyefanya makosa ya kumshambilia Joseph.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na hawana pingamizi la dhamana.

Wakili Kibatala aliiomba Mahakama kutoa masharti nafuu ya dhamana kutokana na asili ya mashitaka hayo.

Pia alidai Malima ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo ni mtu anayetambulika katika jamii kwa kuwa alikuwa Mbunge na Naibu Waziri.

Hakimu Mwijage aliwataka washitakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano. Washitakiwa hao waliachwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Kesi iliahirishwa hadi Juni 15.

Hata hivyo, Wakili Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa katika tarehe ijayo atawasilisha pingamizi kwamba mashitaka ya pili yanayomkabili Malima hayaendani na maelezo yake. 
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo