Makinikia yamzoa Profesa Muhongo


*JPM amtaka ajifikirie, ajitathmini na kuachia madaraka
*Ni miaka miwili tangu alipojiuzulu kwa kashfa ya Escrow

Celina Mathew na Suleiman Msuya

Rais John Magufuli
MIAKA miwili baada ya Profesa Sospeter Muhongo kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini baada ya kuhusishwa na sakata la uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, huenda akalazimika tena kujiuzulu baada ya Rais John Magufuli kumtaka afanye hivyo.

Safari hii, Profesa Muhongo atang’oka baada ya Kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza mchanga wenye madini (makinikia) kutoa taarifa inayoonesha upotevu wa Sh trilioni 1.439 baada ya uchunguzi, kupima mchanga ulio kwenye kontena 277 zilizozuiwa kusafirishwa nje ya nchi tangu Machi.

“Profesa Muhongo nampenda sana, pia ni rafiki yangu, lakini kwenye hili ajifikirie na ajitathmini na bila kuchelewa, nilitaka aachie madaraka,” alisema Rais Magufuli baada ya kupokea taarifa hiyo jana Ikulu, Dar es Salaam.

Mbali na Muhongo ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Rais alitangaza kumsimamisha kazi Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Dominic Rwekaza na kuvunja Bodi ya Wakala huo.

Pia, aliagiza wafanyakazi wote wa TMAA kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini waliohusika na ubadhirifu huo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Magufuli alitoa uamuzi huo baada ya Kamati hiyo aliyoiteua Machi 29 na kuiapisha Aprili mosi, kukamilisha uchunguzi kuhusu mchanga wenye dhahabu.

Kauli ya Rais Magufuli aliyekiri kuwa na urafiki wa karibu na Profesa Muhongo ni pigo kwa msomi huyo ambaye Januari 24, mwaka juzi alimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kujiuzulu baada ya kuhusishwa na Escrow.

Muhongo ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, aliendelea na majukumu yake bungeni hadi Bunge lilipovunjwa kupisha Uchaguzi Mkuu, ambapo alichaguliwa kuwa Mbunge na kisha Rais Magufuli kumteua tena kuwa Waziri wa Wizara hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema uamuzi huo ulitokana na mapendekezo ya Kamati hiyo baada ya kubaini upotevu wa Sh trilioni 1.439, bila hatua yoyote kuchukuliwa na ofisi hizo.

Alisema anamsimamisha Mkurugenzi Mtendaji wa TMAA kwani kwa kiasi kikubwa, amehusika na suala hilo na kuagiza achunguzwe pamoja na wafanyakazi wengine wa Wakala huo.

“Ripoti hii haiwezi kupita hivihivi, maana ikipita tutakuwa watu wa ajabu inabidi nifanye kitu wakati tunasubiri ripoti nyingine, hivyo nimekubali mapendekezo ya Kamati,” alisema Rais Magufuli.

“Wizara imeshindwa kusimamia TMAA na ujenzi wa smelter (mtambo wa kuyeyusha madini), pia haijaweka utaratibu wa kufuatilia makanikia, walishindwa kwa nini, mbona wanasafiri kwenda Ulaya? Unashindwa kuuliza haya makinikia yanapopakiwa hapa yanakwenda wapi upande ndege uyafuate huko!,” alihoji Rais.

Alihoji “wakati hayo yanatokea Kamishna wa Madini alikuwa anafanya na Waziri (Profesa Muhongo), walikuwa wanafanya nini?

“Kwa bahati mbaya niliteua Kamishna mpya wa madini hivi karibuni, siwezi kumhusisha kwenye hili, lakini aliyekuwapo kabla ya huyu, zaidi ya miaka minne aangaliwe alikuwa anafanya nini,” alisema.

Alisema hawezi kuwa na watu waliosomeshwa na nchi halafu wanafanya kazi za kipuuzi na kuvitaka vyombo vya ulinzi kuchukua hatua kwa wahusika wa TMAA.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alisema kuanzia sasa shughuli zote za madini zitahusisha vyombo vya ulinzi na usalama.

“Kuanzia leo vyombo vya ulinzi na usalama vitumike vizuri maana kuna wakati eneo la kutumika polisi hawapelekwi. Kwa nini ulinde kifaru wakati kuna eneo linalosababisha kuwepo vifaru vingi linaachwa,” alisema.

Alibainisha kuwa katika mipaka ya nchi, watu wanasomba madini, na kutaka uwekwe utaratibu ikiwa ni pamoja na kuorodheshwa kwa majina, wahusika kupewa stakabadhi inayoonesha madini husika yanakopelekwa.

Alisema jambo la kushangaza ni kuwa kampuni zinazopelekewa madini zinatajwa kwenye taarifa, lakini kuna makusudi yalifanywa na viongozi wa sekta hiyo kwa kutonunua mtambo wa kuyeyusha madini.

“Cha ajabu, eneo ambalo yanapelekwa madini haijapatikana, kuna tume ya nyuma ilidanganya ilikuwa inasafiri kwenda kule na inaishia hotelini haifikishwi eneo husika,” alisema.

Taarifa

Awali akiwasilisha muhtasari wa Kamati hiyo Mwenyekiti wake, Profesa Abdulkarim Mruma alisema Kamati ilikuwa na kazi ya kuchunguza aina na kiwango cha madini yaliyo kwenye mchanga wa madini unaosafirishwa nje.

Alisema chimbuko la utafiti huo ni kutokana na kutojulikana kwa kiwango cha makinikia na mikataba yake, na kwamba kwenye mchanga huo kumeonekana kiwango kikubwa cha madini.

Alisema hadidu za rejea zilikuwa ni kufanya uchunguzi wa makinikia kwenye bandari ya Dar es Salaam na migodini, kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kujua thamani na aina ya madini yaliyo kwenye makinikia, kuchunguza uwezo wa skena zilizo bandarini na kuchunguza uwezo wa TMAA katika kusimamia makinikia.

Alisema Kamati ilitembelea bandari ya Dar es Salaam, bandari kavu na  migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, ziliko kontena ambazo Kamati ilichukua sampuli za juu na chini na zilizokuwa zigzaga.

Alisema pia ilichunguza uwezo wa skena kupima makinikia na ilikokotoa thamani ya madini yaliyopatikana kwenye makinikia.

Matokeo

Profesa Mruma alisema baada ya uchunguzi, Kamati ilibaini uwepo wa kiasi kikubwa cha dhahabu kwenye makinikia, katika kontena 277 zilizozuiwa ambako kulikuwa na tani saba za dhahabu.

Alisema kontena hizo 277 zilikuwa na dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.147 na kubaini uwepo wa madini ya shaba, fedha, salfa na chuma.

Alisema shaba pekee ilikuwa na thamani ya Sh bilioni 23.3, kukiwa na tofauti kubwa na taarifa ya Serikali iliyoonesha kuwa na thamani ya Sh bilioni 13.

Pia, ilibaini uwepo wa fedha ya thamani ya Sh bilioni 2.1, tofauti na taarifa ya Serikali iliyoonesha thamani ya Sh bilioni moja.

Alisema Kamati pia ilibaini uwepo wa salfa ya thamani ya Sh bilioni 1.9 na madini haya hayakuwa kwenye ukokotoaji wa mrabaha.

Aliongeza kuwa Kamati ilibaini uwepo wa madini ya chuma yenye thamani ya Sh bilioni 2.3, na madini mkakati ambayo kwa sasa yanahitajika sana duniani yakiwa na thamani ya kati ya Sh bilioni 129.5 na Sh bilioni 261.5.

“Thamani ya madini yote katika makinikia kwenye kontena 277 yaliyochunguzwa Kamati ilibaini kuwa na thamani ya Sh trilioni 1.339, ambazo Serikali haipati hasa senti moja na hayamo kwenye ukokotoaji wa mrabaha,” alisema.

Profesa Mruma aliongeza kuwa Kamati iligundua madini mengine mengi ambayo hayarekodiwi kwenye nyaraka za Serikali.

Pia, ilibaini kuwa TMAA haifungi rakili kwenye kontena kuonesha viwango vya madini, ambapo Kamati ilibaini kuwa ufungwaji huo hufanyika wakati wa kusafirisha kontena.

Mbali na hayo ilibaini kuwa skena za bandarini hazina uwezo wa kubaini utoroshwaji wa madini hayo.

Mapendekezo

Kamati iliiomba Serikali kusitisha usafirishaji wa mchanga nje ya nchi hadi mrabaha stahiki utakapolipwa kwa kuzingatia thamani stahiki.

Aidha, iliitaka Serikali ihakikishe mitambo ya kusafisha makinikia unajengwa nchini na TMAA ifunge rakili baada ya mchanga kupakiwa kwenye kontena na pia ipime metal zote kwenye makininia.

Mengine ni TMAA ipime viwango vyote vya makinikia na madini kwenye mbale bila kujali taarifa ya msafirishaji, hali ambayo itasaidia Serikali kupata mrabaha.

Aidha, Serikali iwachukulie hatua watendaji wa TMAA na wizara husika, na iweke mfumo wa kushitukiza kwenye udhibiti wa madini, na itumie wataalamu wa mionzi kwenye skena za bandarini, ili kuona kama zinaweza kufanya kazi.

Kamati hiyo ambayo iliongozwa na Profesa Mruma iliundwa pia na Profesa Justinian Ikangula, Profesa Joseph Bushweshaiga, Dk Yusuf Ngenya, Dk Joseph Philip, Dk Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.

Uundwaji wa Kamati hizo ni mkakati wa Rais Magufuli kujiridhisha na kupata ukweli kuhusu mchanga wa madini unasafirishwa kutoka kampuni za uchimbaji dhahabu nchini na kupelekwa nje ya nchi kwa kinachodaiwa ni kwenda kuchenjua.

Rais Magufuli amekuwa akilalamikia utaratibu huo wa kusafirisha mchanga wa dhahabu hata kabla ya kuwa Rais, jambo ambalo sasa aliamua kulivalia njuga baada ya kuwa mkuu wa nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo