Warioba, Makinda wamzungumza Sozigwa


Claudia Kayombo

Jaji Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda wamemzungumzia  marehemu Paul Sozigwa wakimtaja kuwa mfano wa uadilifu kwani alilitumikia Taifa kwa uadilifu mkubwa.

Walitoa kauli hiyo juzi jioni muda mfupi baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Sozigwa aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini wakati wa uhai wake.

Baadhi ya nyadhifa alizowahi kushika ni pamoja na mwandishi wa habari wa Mwalimu Julius Nyerere na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Utalii.

Sozigwa aliagwa juzi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mtoni Mtongani na kuzikwa jana kwenye makaburi ya Wamisionari wa KKKT Kisarawe, Pwani.

“Tumezoea kusema kiongozi mzuri anatakiwa kuwa mzalendo, mwenye maadili na mchapakazi, Sozigwa alikuwa na sifa hizo, aliipenda sana nchi yake na aliitumikia kwa uadilifu mkubwa,” alisema Warioba.

Alibainisha kuwa Sozigwa alizingatia misingi yote ya uongozi bora na hivyo kuwa mtu wa mfano, na kwamba Taifa limepoteza mtu mwadilifu.

“Ripoti yangu ya rushwa ya mwaka 1996 ilionesha kuwa viongozi ni watu wanaojihusisha na rushwa, siku moja tulikuwa katika chumba kimoja watu 160 wakasema kiongozi ambaye hajawahi kupokea au kuomba rushwa ajitokeze, alikuwa Sozigwa peke yake na ni kweli alichosema,” alibainisha Jaji Warioba.

Makinda alisema kama kuna mtu aliwahi kuishi huku akizingatia misingi ya maadili mema na uaminifu katika nchi hii ni Sozigwa.

Hata hivyo, alisema hakujua maisha yake ya kiimani, lakini baada ya kusikia taarifa kanisani hapo juzi wakati wa ibada ya kumwombea, anaamini kuwa alifanikiwa kufanya hayo kwa sababu alikuwa mcha Mungu.

“Alikuwa ni mtu mwenye upendo, alikuwa tayari kutembea hata kwa miguu licha ya kuwa alikuwa na usafiri wake, hakuwa mtu wa kujikweza, pia alikuwa mwenye ushauri, alishauri bila woga,” alibainisha.

Hata hivyo, alisema vijana wengi hawamfahamu Sozigwa na hivyo ni vigumu kuiga maadili mema kutoka kwake, huku akionesha masikitiko yake kuwa hakuna hata vitabu vinavyoelezea maisha ya viongozi waadilifu wa Taifa.

“Vijana wanaangalia mitandao tu, hawamjui Sozigwa, na hakuna mahali ambako historia ya Taifa hili inayoonesha watu hawa ili kizazi cha sasa na kijacho kijifunze kutoka kwao,” alibainisha Makinda.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula alisema Sozigwa aliaminiwa sana na Mwalimu Nyerere na kwamba hilo tu ni ishara tosha ya uaminifu wake kwa Taifa.

“Binafsi kwa Sozigwa nimejifunza uaminifu wake kwa Taifa, yeye pia aliaminiwa sana na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hadi kuaminiwa na Mwalimu lazima uwe na tabia mnayoendana,” alisema Mangula.

Sozigwa ambaye katika uhai wake aliwahi kuwa pia Katibu Mkuu Wizara ya Habari na Utalii mwaka 1963-67, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe wa kwanza Mwafrika mwaka 1959, alizaliwa Februari 23, 1933 na kufariki dunia alfajiri ya Mei 12.

Ameacha mjane Monica, watoto sita, wajukuu 13 na vitukuu watatu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo