Tizeba: Kilimo hakiepukiki azma ya viwanda


Mwandishi Wetu
Dk. Charles Tizeba

WAZIRI wa Kilimo, Chakula, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, amesema kilimo kina mchango mkubwa katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa kati na viwanda.

“Kilimo hakiepukiki katika dhamira ya Serikali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwani malighafi nyingi zitatokana na mazao ya kilimo,” alisema Waziri Tizeba katika Mkutano wa Kumi wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Dk. Tizeba aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba Tanzania ya viwanda inawezekana na kushauri uwekezaji mkubwa ufanyike pia kwenye kilimo.

“Tumefanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo ilikuendana sambambana azma ya serikali ya viwanda. Kwa mfano tumetoa tozo mbalimbali ili kuchochea uzalishaji,” alisema.

Dk. Tizeba alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. Magufuli imechukua hatua mbalimbali madhubuti kuhakikisha kuwa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea inashuka na kumpa nafuu mkulima.

“Bei ya mbolea ni ghali sana na sasa tumeangalia mnyororo wa upatikanaji wake,” alisema.

Alieleza kwamba jitihada za makusudi zimeshachukuliwa kuhakikisha bei ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo zinashuka na kutoa nafuu kwa mkulima.

Kwa mujibu wa Dk. Tizeba, tafiti nyingi zinaonyesha kuwa kutangaza zabuni ya kuagiza mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement) kutasaidia kushusha bei ya mbolea nchini na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.

“Tumeandaa pia utaratibu wa utunzaji wa mazao ya msimu ilikuyaongezea thamani staili mazao hayo,” alisema.

Waziri Tizeba alisema kumekuwa na upotevu wa asilimia 48 ya mazao yote yanayovunwa hapa nchini na wizara yake inaangalia namna ya kuzuia upotevu huo.

Kwa upande wa mbegu Tizeba alisema mbegu zinazozalishwa hapa nchini zimekuwa ghali sana ukilinganisha na zile zinazotoka nje.

“Utashaanga mbegu kwa mfano zinazoingizwa toka nje zitaunza 1,500 kwa kilo lakini za hapa ndani zitauzwa 7,000, lakini pia mbegu hizo hazitoshi wala kuwafikia wakulima wote kwa wakati,” alisema.

Alibainisha kwamba Serikali imeshapitia na kupitisha kanuni zitakazotumika kupitisha mbegu ambazo zitakazokuwa zinatumika ambapo hapo awali ilikuwa inachukua miaka mitatu na sasa itakuwa ni mwaka mmoja tu.

Mkutano huo wa Baraza ambao ulishirikisha sekta za umma na biashara ulibeba maudhui ya Tanzania ya Viwanda; Ushiriki wa Sekta Binafsi ambapo uliongozwa na mwenyekiti wake Rais John Magufuli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo