Waliomaliza kidato 6 waitwa JKT


Mwandishi Wetu

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limechagua vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka huu kutoka shule zote Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo yanayotolewa na Jeshi hilo kwa mujibu wa sheria.

Aidha, limewapangia kambi watakazokwenda kupewa mafunzo kwa miezi mitatu na kuwataka kuripoti kuanzia Mei 25 hadi 30.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano wa JKT, vijana waliochaguliwa wamepangiwa kambi za JKT Rawamkoma, Mara; JKT Msange,Tabora; JKT Ruvu, Pwani na JKT Makutupora, Dodoma.

Zingine ni JKT Mafinga, Iringa; JKT Mlale, Ruvuma; JKT Mgambo; JKT Maramba,Tanga; JKT Makuyuni, Arusha; JKT Bulombora, Kigoma, JKT Kanembwa, Kigoma na JKT Mtabila, Kigoma.

Iliongeza kuwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wanatakiwa kuripoti kambi ya JKT Ruvu iliyo Mlandizi, Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.

Aidha, liliwataka vijana hao kuripoti na vifaa kama bukta za bluu nyeusi yenye mpira kiunoni na mfuko nyuma, urefu unaoishia magotini isiyo na zipu, raba za michezo za kijani au bluu, shuka mbili za kulalia za bluu ya  bahari pia.

Vingine ni soksi ndefu za rangi nyeusi, nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi, suti ya michezo ya kijani au bluu na nauli ya kwenda kambini na kurudi.

Taarifa ilisema Mkuu wa JKT anawakaribisha vijana wote waliochaguliwa ili kujiunga na wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa.

Aidha, ilisema orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa maeneo ya kambi za JKT walizopangiwa na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo