Manchester yalipuliwa kigaidi, 22 wauawa


MANCHESTER, Uingereza

TAKRIBAN watu 22wakiwamo watotowamepoteza maisha huku 59 wengine wakijeruhiwa katika shambulio la kujitoa mhanga, lililolenga vijana waliokusanyika kwenye uwanja wa michezo wa Manchester Arena usiku wa kuamkia jana.



Shuhuda wa shambulio hilo baya kutokea tangu lingine la Julai 7 alisimulia alivyoona nati na bolti zilivyojeruhi vijana waliokuwa wakiburudika baada ya bomu hilo kulipuka katika eneo la wazi, kati ya uwanja huo na kituo cha treni cha Victoria, muda mfupi baada ya onesho la muziki wa msanii wa kizazi kipya, Ariana Grande kumalizika.

Picha moja ya tukio hilo, ilionesha miili ya marehemu na majeruhi kwenye eneo hilo lililofurika watu wakiondoka baada ya onesho hilo la muziki kumalizika.

Polisi jana asubuhi walithibitisha, kwamba mtu aliyejitoa mhanga alifia ndani ya uwanja huo baada ya bomu hilo kulipuka.

Mlipuko ulipotokea, vijana waliojawa hofu walibanana kwenye malango ya uwanja huo unaobeba watu 21,000. Mashuhuda waliyaelezea mauaji hayo   yaliyofanya eneo hilo kuonekana kama ‘ukanda wa vita’.

Polisi wenye silaha, kikosi cha kutegua mabomu na magari ya dharura walifurika eneo la tukio hilo lililotokea saa 4.35 usiku.

Muda mfupi baada ya saa 7.30 usiku, kitu kingine kama mlipuko kilionekana kwenye bustani za Kanisa Katoliki karibu na uwanja huo wa Manchester Arena, lakini baadaye polisi walithibitisha kwamba kitu hicho kilikuwa ni vazi la kawaida.

Maofisa wa usalama wa Marekani walisema wenzao wa Uingereza walimtambua mwanamume ambaye wanaamini ndiye aliyejitoa mhanga.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari saa 9 alfajiri, Konstebo Mkuu wa Polisi wa Manchester, Ian Hopkins alithibitisha kwamba kikosi chake kinachukulia tukio hilo kama shambulio la kigaidi.

Saa moja baadaye, nyota huyo wa muziki wa Marekani, Grande, ambaye alinusurika katika shambulio hilo, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba ‘amenyong’onyezwa’.

“Kutoka moyoni mwangu, nasikitika sana sana. Sina cha kusema,” aliongeza mwanamuziki huyo wa kike. Meneja wake, Scooter Braun alisema: “Tunaomboleza watoto.”

Shuhuda Evie Brewster, aliyepelekwa na mama yake kwenye onesho hilo ikiwa ni mara yake ya kwanza maishani kuhudhuria, aliiambia MailOnline jinsi kishindo cha mlipuko huo kilivyosikika katika eneo lote hilo la uwanja mwishoni mwa onesho.

“Ariana Grande alikuwa ndio kwanza amemaliza na wimbo wake wa mwisho na kushuka jukwaani ndiyo mara ukasikika milio mkubwa wa mlipuko,” alisema.

“Ghafla kila mtu alianza kulia na kukimbilia langoni. Tuliweza kusikia ving’ora vya Polisi na magari ya wagonjwa. Ilitisha. Kulikuwa na maelfu ya watu wakijaribu kutoka nje kwa pamoja. Walikuwa wakilia na kupiga kelele. 

“Eneo lote liligubikwa harufu ya moshi na moto. Mlipuko huo ulikuwa kama umetokea ndani ya jengo mahali fulani.”

Hopkins alisema jana, kwamba anaamini mtu huyo aliamua mwenyewe kutekeleza shambulio hilo na walikuwa (polisi) wakijaribu kubaini kama alikuwa na mtandao.

Aliongeza kuwa watoto ni “miongoni mwa marehemu” na kusema jana asubuhi: “Hili limekuwa ni tukio la kutisha sana tulilopata kushuhudia katika Manchester Kuu na ambalo hakuna mtu aliyekuwa akitarajia kulishuhudia.

“Familia na vijana wengi walikuwa wamekwenda kuburudika kwenye onesho hilo kwenye uwanja wa Manchester Arena, lakini wamepoteza maisha yao.

“Mawazo yetu yako kwa watu 22 ambao hivi sasa tunajua wamepoteza maisha, na watu 59 waliojeruhiwa na pia kwa wapendwa wao.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo