Vijana 190 kushiriki mkutano wa dipliomasia, uongozi

Mary Mtuka

MKUTANO Mkuu Kivuli wa Umoja wa Mataifa (TIMUN) unatarajiwa kufanyika kati ya Mei 22 na 26 mwaka huu jijini Arusha ukilenga kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya diplomasia, uongozi na namna umoja huo unavyofanya kazi.

Mkutano huu unaoongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuwawezesha Vijana katika Diplomasia na Uongozi” unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya vijana 190 kutoka mataifa mbalimbali duniani ukiyashirikisha mataifa 35.

Akizungumza  Dar es Salaam jana Mratibu wa mkutano huo, Tajiel Urioh alisema baadhi ya mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na afya ya uzazi na uzazi wa mpango, demokrasia na amani katika nchi zinazoendelea, matumizi ya nishati mbadala na isiozalisha hewa ukaa pamoja na elimu kwa maendeleo endelevu.

“Majadiliano ya mwaka huu yatajikita katika mada kuu ya kuwawezesha vijana katika Diplomasia na Uongozi Mada hii inalenga kuwezesha ushiriki wa vijana na kuwajengea uwezo kwenye masuala ya Diplomasia na Uongozi kwa kuwapa mafunzo ya vitendo katika mada ngumu ambazo zitawaongezea ujuzi wa majadiliano na kufikia muafaka wa masuala mtambuka yanayogusa masilahi ya mataifa.

Alisema kuwajengea uwezo vijana katika masuala hayo kutasaidia kuwa na mataifa yenye vijana wenye uwezo wa kuamua mambo yao wenyewe.

Aliongeza kuwa katika mkutano huo wajumbe watawasilisha maazimio mbalimbali yenye manufaa katika maisha yao ya kila siku na watu wanaowazunguka katika jamii zao.

"Ni matarajio yangu kwamba watakuwa tayari kujifunza kuendana na mada kuu lakini pia kubadilishana mawazo na wajumbe wengine na kutengeneza mtandao wa vijana wenye fikira wanazoendana nazo," alisema Urioh.

Alisema kuhusu tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana  wamekuwa wakijadiliana kuona kwanini kuna tatizo la ukosefu wa ajira ambapo waligundua kuwa husababishwa na mfumo wa elimu usiowajengea vijana uwezo wa kujiajiri.

“Kuhusu suala la matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa  kwa vijana, hivyo tunalikemea kwa sababu huwaneemesha watu wachache na kupoteza vijana ambao ndiyo nguvu kazi” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa Tanzania (YUNA), Arafat Bakir, alisema kuwa lengo lni kuwashirikisha vijana katika masuala ya Umoja wa mataifa ambapo wamefanikiwa kufikia zaidi ya vyuo vikuu 35 na shule mbalimbali za sekondari kuhakikisha vijana wengi wanashiriki katika malengo ya maendeleo.

“kutokana na azma hiyo tumekuwa tukifanya mkutano huu katika mikoa mbalimbali ili kuwafikia vijana wengi zaidi” alisema Bakir.

Kwa upande wake Ofisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, Stella Vuzo, alisema kuwa wamekuwa wakiwaunga mkono vijana hao kwa kuwapa fedha na kuwashauri.

Alisema wamefanya mikutano mingi na wamekuwa imara katika uongozi na mafanikio yanaonekana, hata Francis Nkuhi (mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki) ni matokeo ya mkutano huu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo