Serikali yasisitiza ubora barabara ya Mafinga – Nyigo


Mwandish Wetu

WAKANDARASI wa kampuni ya China Civil Engeneer Construction Cooporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga hadi Nyigo yenye kilomita 74.1 na (CRSG) anayejenga sehemu ya Nyigo hadi Igawa yenye urefu wa kilomita 63.8, wametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi ili barabara hizo zikamilike kwa wakati.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Iringa Daniel Kindole kuhakikisha ubora wake unakidhi malengo ya Serikali.

“Barabara hii ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM inaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Zambia na Malawi, hivyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi, sasa ni lazima isimamiwe kikamilifu ili idumu kwa muda mrefu”, alisema.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Tanroads, Kindole alisema tayari kilomita 18 kati ya 74.1 katika sehemu ya kwanza ya Mafinga hadi Nyigo imeshawekwa lami na mkandarasi ameunda timu tatu ili kuharakisha ujenzi huo.

“Ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Igawa unahusisha mikoa mitatu ambapo kilomita 74.1 ziko katika mkoa wa Iringa, kilomita 52 zipo Njombe na kilomita 12 ziko Mbeya hivyo mimi pamoja na wenzangu tumejipanga kuhakikisha barabara hii inakamilika Novemba mwakani kama ilivyopangwa”, alisisitiza.

Meneja Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya Mafinga hadi Nyigo ambayo ina kilomita 74.1 Richard Guo amemhakikishia naibu waziri kwamba kasi yao ya ujenzi ni nzuri na barabara hiyo imeimarishwa ili kukidhi mahitaji na itakamilika kwa wakati.

Zaidi ya sh. bilioni 116 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza yaani Mafinga- Nyigo kilomita 74.1 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo