Wabunge wataka Sagcot iongeze wigo wa huduma


Mwandishi Wetu, Dodoma

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Ardhi na Maji, wameshauri Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), kutanua wigo wa shughuli zake  ili wakulima wengi wadogo wanufaike nje ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mjini Dodoma, wajumbe walipokea taarifa ya shughuli zinazofanywa na SAGCOT kwa lengo la kujua changamoto ambazo shirika hilo linakabiliana nazo.

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha aliwakaribisha wajumbe hao na kusisitiza kuwa wao ndiyo sauti ya SACGOT.

"Naamini Kamati hii ya Bunge itapata taarifa ya shughuli za SACGOT na hivyo kuwa katika nzuri ya kuilezea,"alisema.

Mwenyekiti wa Kamati, Dk. Mary Nagu, amesema amevutiwa na juhudi za SAGCOT katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hali inayoonyesha wakulima wadogo sasa wana fursa nyingi za kujinufisha kupitia kilimo kinyume na mazoea kuwa kilimo ni shughuli ya watu wa chini.

“Naona hata hiki kikao kimekuwa kifupi naomba tuandae kingine ili tupate elimu zaidi kuhusiana na shughuli mnazofanya kuwaamsha wakulima na kuona fursa, vilevile tutajipanga kamati tutembelee kongani mlizoainisha ili tuangalie namna mazao yanavyolimwa na njia zinazotumika kuongeza uzalishaji.

“Kingine nilichojifunza ni fursa za wafanyabiashara na wawekezaji kupitia kilimo, ni wazi wawekezaji wanategemea kwa kiasi kikubwa mavuno na mazao bora ili kuzalisha bidhaa nzuri. Uchumi wa viwanda unategemea kilimo chenye tija na nyinyi mnatuhakikishia kuwepo tija hiyo,” alisema Dk. Nagu.

Wajumbe walitaka ziwepo njia nzuri za kuhifadhi mazingira ili kupata maji ya uhakika siku zote na udongo wenye rutuba kwa ajili ya kilimo bora.

 Wameishauri SAGCOT kuongeza elimu juu ya namna bora ya kutunza mazingira katika kongani wanazofanyia kazi.

Awali akiwasilisha taarifal ya Sagcot juu ya shughuli zake, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bwana Geoffrey Kirenga, amesema lengo lao kubwa ni kubadili sekta ya kilimo kutoka kilimo cha mazoea na kuwa kilimo cha biashara pamoja na kuongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo.

Alisisitiza mambo wanayoyaangazia katika kongani kuwa ni kudhibiti matumizi ya maji na ardhi, kuongeza uzalishaji wa mazao katika hekta.  Suala lingine ni kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ili kupata faida na kukuza uchumi wa nchi kupitia kilimo.

“Tulipoanzisha mpango huu miaka sita iliyopita tulikuwa na mipango mingi na baadhi imeshaanza kuzaa matunda.  Kutokana na mafanikio tuliyopata,  tunatazamia kuwatoa katika umasikini zaidi ya watu milioni mbili.

Hadi kufikia 2030 Sagcot inatwania hekta 350,000 zizalishe mazao ya kilimo kwa faida “na tuachane na kilimo cha mazoea ambapo mkulima faida yote anaitumia kwa ajili ya chakula na mavazi tu.”

Katika kipindi hicho SAGCOT inapanda kuzalisha ajira mpya 420,000 zitokanazo na kilimo. “Hapa tunazungumzia wauzaji pembejeo, wauzaji bidhaa za kilimo ikiwemo chakula na wakulima wenyewe,” alisema Bw. Kirenga.

SAGCOT imeainisha kongani sita ambazo ni Ihemi inayojumuisha mikoa mitatu ya Mbeya, Iringa na Njombe, kongani ya Kilombero inayohudumia Mkoa wa Morogoro, Kongani ya Mbarali (Mbeya na Songwe), Kongani ya Sumbawanga (Rukwa), Kongani ya Ludewa (Ruvuma) na Kongani ya Rufiji (Pwani).

Hata hivyo kwa sasa kongani inayofanya kazi ni Ihemi ambayo kwa ujumla wake inasimamia wakulima wa Nyanya, Mchele, Viazi, Soya, Mahindi na ufugaji kwa ajili ya maziwa. Katika mikoa hiyo kwa ujumla wilaya sita ndizo zinazoshughulikia kilimo hicho na fugaji ambazo ni Wilaya ya Iringa Vijijini, Kilolo, Mufindi, Njombe Vijijini,

Wanging’ombe na Njombe Mjini.

Wafadhli wakubwa wa SACGOT ni Serikali ya Tanzania,Shirika la misaada la Uingereza (UK Aid),Shirika la misaada la Marekani(USAID),Benki ya Dunia (WBG),Ubalozi wa Norway,Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na AGRA.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo