Muhongo agoma kusaini leseni inayokandamiza mzawa


Veronica Simba, Dodoma

Profesa Sospeter Muhongo
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amekataa kusaini maombi la uhamishaji wa leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya shaba namba ML 571/2017 kutoka kwa Mtanzania David Kayongoya kwenda kampuni ya Mechanized Minerals Supreme Mining Limited inayomilikiwa na raia wa China.

Profesa Muhongo alikataa kusaini leseni hiyo ya eneo la ukubwa wa kilometa 0.43 za mraba lililoko Fufu, Chwamwino, Dodoma, baada ya kubaini kuwa Mtanzania anayetaka kuhamishia leseni hiyo kwa raia wa China, hatanufaika kwa kiwango kinachoridhisha.

Akizungumza na wawekezaji wa sekta ya madini, waliofika wizarani juzi, kusainiwa leseni zao za uwekezaji, Profesa Muhongo alisisitiza kuwa ni lazima wawekezaji katika sekta hiyo wazingatie maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla, wakati wanapowekeza.

Waziri Muhongo alimwagiza mwekezaji huyo wa China kujadiliana kwa mara nyingine na Mtanzania mwenye eneo ili kuhakikisha ananufaika ipasavyo na uwekezaji huo.

“Ili niweze kusaini leseni hii, rudini mezani, mzungumze na kukubaliana ili David aweze kunufaika. Hatuwezi kukubali kuona Watanzania wakidhulumiwa namna hii,” alisisitiza Waziri.

Awali, ilielezwa kuwa mkataba wa mauziano ya leseni husika unaonesha kuwa David amepokea Sh milioni 30. Waziri alipotaka kujua endapo kuna manufaa mengine ambayo David atapata, alielezwa kuwa ataajiriwa katika kampuni hiyo kama kibarua, ndipo Waziri akakataa kusaini leseni husika.

Ili kuhakikisha suala hilo linatekelezwa ipasavyo, Profesa Muhongo alimwagiza Kamishna wa Madini nchini, Benjamin Mchwampaka, kujiridhisha kwa kupokea ahadi za maandishi kutoka kwa mwekezaji yeyote anayeomba leseni, namna ambavyo atazingatia maslahi ya nchi, kabla ya kumpatia leseni anayoomba.

Kamishna Mchwampaka, pamoja na kuahidi kuzingatia na kutekeleza agizo la Waziri; aliwataka wawekezaji hao kuzingatia kanuni na miongozo ya uwekezaji kama inavyobainishwa katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo