NBC yaanza kutoa gawio kwa Serikali


Mwandishi Wetu

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa gawiwo la Sh. bilioni 1.7 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa zake.

Hundi ya kiasi hicho cha fedha alikabidhiwa kwa  Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango kwa niaba ya Waziri Mkuu katika hafla ya  kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo.

Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika Hoteli ya Morena Mjini Dodoma ambako imebainishwa kuwa ni mara ya kwanza kwa benki hiyo kutoa gawiwo.

Dk Mpango aliishukuru benki hiyo kwa kuanza kutoa gawiwo kwa wanahisa wake baada ya ukame wa muda mrefu na kuelezea matumaini yake kwamba kiasi cha gawiwo kitaongezeka zaidi miaka ijayo.

Hata hivyo, alizitaka benki zote nchini kupunguza riba za mikopo inazotoza kwa wateja wao hasa baada ya Benki Kuu ya Tanzania-BOT kupunguza riba za mikopo kwa mabenki kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12.

“Hii itakuwa mara ya kwanza kwa benki hiyo kutoa gawiwo kwa wanahisa wake katika kipindi cha miaka 9 baada ya kuanza kupata faida ya uwekezaji wake hapa nchini,” alisema.

Alizitaka pia taasisi za fedha nchini, kuwekeza fedha katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo kwa njia ya mikopo kwa wateja wao kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitakavyosisimua uchumi na kukuza ajira nchini.

Mpango alipongeza juhudi zilizofanywa na benki hiyo kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mtandao wa malipo ya kielektroniki ikiwa ni maagizo ya Serikali kwamba malipo yote ya Serikali yafanyike benki au kupitia miamala ya kielektroniki

“Nimefurahi kuthibitishiwa kwamba tangu Julai Mosi 2016 hadi kufikia Aprili 30, 2017, NBC imekusanya fedha za Serikali na kuzituma kielektroniki katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jumla ya Sh. billioni 991” aliongeza Dk. Mpango.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Nehemiah Mchechu, alieleza mkakati wa benki hiyo ni pamoja na kutoa mikopo ambapo kwa sasa imetoa mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 1 na itaendelea kusogeza huduma zake kwa wananchi na wafanyabiashara wa kati na wa chini kabisa.

“Mwaka jana benki yetu imepata faida ya zaidi ya sh.bilioni 13 na katika mkutano mkuu wa wanahisa tuemekubaliana kutoa gawiwo kwa wawekezaji” aliongeza Mchechu.

Alisema NBC inamilikiwa na wabia watatu, wakiwemo kundi la Mabenki ya Barclays (ABSA Group ltd) ya Afrika Kusini, inayomiliki hisa nyingi zaidi, Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 30 huku Benki ya Dunia (WB), kupitia Taasisi yake ya Fedha ijulikanayo kama The International Finance Corporation (IFC), ikiwa na hisa asilimia 15.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo