Ushiriki uwe nyenzo katika hifadhi ya msitu wa Ruvu Kusini

Mashaka Mgeta

Mashaka Mgeta
MWISHONI mwa wiki iliyopita, Jumuiko la Maliasili Tanzania kupitia kampeni ya Mama Misitu, iliwakutanisha wahariri na waandishi waandamizi katika semina na ziara iliyowafikisha kwenye maeneo yenye msitu wa Ruvu Kusini mkoani Pwani.

Ni mafunzo yaliyoibua hitaji la ‘nguvu zaidi’ katika kuchagiza kasi ya vyombo na waandishi wa habari kuelimisha, kutetea na kutoa taarifa zinazohusiana hifadhi ya misitu.

Takwimu zinazotokana na tathmini ya rasilimali za misitu iliyofanyika mwaka 2013, zinaonesha kuwa tani milioni moja za mkaa kila mwaka hutokana na ukataji wa misitu iliyopo kwenye eneo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta milioni 48.1 nchi nzima.

Pia utafiti uliofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ulionesha kuwa katika uhifadhi, Tanzania inapoteza hekta 400,000 za misitu kila mwaka kupitia matumizi ya kuni, mkaa, mbao, ujenzi na uchomaji moto misitu.

Zipo athari nyingi zinazotokana na uharibifu wa misitu kiasi kwamba hata zikiorodheshwa na kufafanua hapa, nafasi iliyopo kwenye safu hii haitatosha.

Lakini misitu ikiwa ni sehemu ya ‘maumbo’ ya mazingira yanayohitaji kutunzwa, ina manufaa lukuki katika maisha ya binadamu na mimea. Misitu ni makazi, hifadhi ya vyanzo vya maji, `kivutio’ cha mvua kunyesha, hifadhi ya rasilimali kama madini na mahali ambapo shughuli za kibinadamu zinafanyika.

Ndio maana ziara iliyowafikisha wahariri na waandishi wa habari waandamizi kwenye msitu wa Ruvu Kusini, haikuwa mfano wa utalii wa ndani, bali ni kupata ukweli wa namna msitu huo, miongoni mwa mwingine, unavyohifadhiwa, kunufaisha jamii zinazoishi kuuzunguka, changamoto zilizopo na namna bora ya kuzitatua.

Kwa bahati nzuri, wakazi wa vijiji 11 vya wilaya za Kibaha na Kisarawe vinavyouzunguka msitu wa Ruvu Kusini wamenufaika kupitia mafunzo yaliyotolewa na waelimishaji wa kampeni ya Mama Misitu, hivyo kuwa na uelewa mpana wa masuala yanayohusu sheria, kanuni na sheria ndogo, miongoni mwa mambo muhimu ya ushiriki wao katika uhifadhi wa msitu huo.

Meneja wa Msitu wa Ruvu Kusini wa TFS wenye ukubwa wa hekta 30,633, Nassoro Mzava, anavitaja vijiji hivyo kuwa ni Soga, Boko Mnemela, Kibomwendwa, Malangalanga, Mtamba, Kifuru, Mpiji, Chakuge, Kisanga Kona, Sangwi na Kipange.

Latifa Felex, ni mjumbe wa kamati ya ardhi na mazingira ya kijiji cha Soga, anasema kabla ya kupata mafunzo kupitia Mama Misitu, jamii zinazoishi kuuzunguka msitu huo hazikutambua manufaa yam situ, badala yake zikawa sehemu ya matukio yaliyochangia uharibifu wake.

Anasema ulinzi na uhafadhi wa msitu wa Ruvu Kusini ilikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyofikiriwa kuwa kati ya majukumu ya Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama. “Lakini baada ya kupata kuwezeshwa kupitia mafunzo ya Mama Misitu na wadau wengine ikiwamo Serikali, tumetambua wajibu wetu na sasa tunashiriki katika ulinzi na uhafadhi wa msitu,” anasema.

Hata hivyo, mchakato wa kuwapo ushiriki timilifu bado haujafikia kilele chake kutokana na changamoto kadhaa ikiwamo ya kutokuwapo kwa mpango wa usimamizi uliopitishwa na kutosainiwa kwa mikataba ya makubaliano kati ya TFS na vijiji vinavyozunguka msitu wa Ruvu Kusini.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipangige, Shomari Juma anasema kukosekana kwa ushirikiano madhubuti kati ya wananchi na TFS kunazorotesha ufanisi katika maeneo tofauti yenye tija, miongoni mwa hayo ikiwa ni uwasilishaji wa tozo zinazotokana na mazao ya misitu kwa vijiji husika.

“Hivi sasa hakuna mfumo rasmi unaotambulika kupitia makubaliano ambayo bado hayajasainiwa, hivyo marejesho yanayofanyika sasa yanategemea zaidi utashi wa TFS, hali ninayodhani inaweza kufifisha ari ya wanajamii kushiriki ulinzi na uhifadhi wa msitu huo,” anasema.

Lakini Mzava anasema ingawa changamoto hiyo (iliyotajwa) ipo, mfumo wa makusanyo na matumizi ya fedha za umma kupitia TFS inasababisha mchakato wa kurejesha fedha vijijini kuchukua muda mrefu, hali inayoweza kufifisha ari ya ushiriki wa wananchi kuhifadhi na kuulinda msitu huo.

Anafafanua kwamba fedha zinazohusika katika ‘eneo’ hilo ni zinazotokana na faini zinazotozwa kwa watu wanaokutwa wakiharibu misitu na ambazo kiasi chake kinatozwa kutokana na tofauti za mazingira na sababu zilizoainishwa kwenye sheria, kanuni na miongozo inayohusiana na misitu.

kukwama kwa makubaliano ama mikataba kati ya TFS na vijiji vinavyouzunguka msitu wa Ruvu Kusini, kunachangiwa pia na vijiji husika kushindwa kufanya mikutano ya kijiji ili kuwapa fursa wananchi kujadili na kupitisha maazimio yanayohusiana na mikataba husika.

Kwa mujibu wa Mzava, kiasi cha vijiji vitano kati ya 11 vilivyopo, vimefanikisha kuitisha mikutano hiyo na kupitisha makubaliano ya ushirikiano na kwamba vijiji vilivyobaki havijafikia hatua hiyo.

Pia Mzava anasema licha ya hali hiyo, TFS inaendelea kushirikiana na kamati za ardhi na mazingira za vijiji vyote kufanya doria kwa kadri inavyohitajika, ingawa katika mazingira na nyakati kadhaa, wajumbe hao hawashirikishwi hasa katika kupanga ratiba ya siku ya doria.

“Imetokea mara kadhaa kwamba wajumbe wa kamati hizo wanapojulishwa kuhusu siku na wakati wa doria, wanazipenyeza taarifa hizo kwa wahusika na hivyo kuwapa mwanya wa kuikwepa doria,” anasema.

Afisa Mwandamizi wa TSF, Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Emmanuel Msofe, anasema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutathmini na kuchunguza mazingira misitu ili kuchapisha ama kutangaza habari zenye tija na ufanisi unalenga katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali hiyo.

Msofe anasema hatua hiyo itafikiwa waandishi wa habari watapata uelewa mpana, uzoefu na ushiriki katika masuala yanayohusu misitu, ili kuzifanya habari zao kuwa zenye kuleta mijadala na mabadiliko chanya.

Msofe anaeleza namna misitu inavyotegemewa katika uhai wa viumbe na shughuli za binadamu na kwamba hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inazipitia ili kufanya maboresho kwenye Sheria ya Misitu ya mwaka 1998, hali itakayotokea pia kwenye kanuni zake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo