Abiria wa TRL wasota Morogoro kwa saa nne


Mwandishi Wetu

ABIRIA wa treni ya Reli ya Kati kutoka Bara kwenda Dar es Salaam  wamesota kwa saa nane Morogoro wakihamishia mizigo kwenye mabasi baada ya daraja la Mazimbu kusombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Abiria hao zaidi ya 500 waliotoka Kigoma Jumatatu saa 6 mchana, walishuka kwenye treni hiyo eneo la Lukobe usiku wa kuamkia jana na kupakua mizigo kwenye treni hiyo na kuipakia kwenye mabasi na kwenda Morogoro Mjini ili kupanda treni nyingine ya kwenda Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa abiria waliozungumza na gazeti hili jana, walitumia saa nane kuhamisha mizigo na kutoka eneo hilo hadi stesheni ya Morogoro huku wakinyeshewa mvua.

"Tulifika Lukobe saa nne usiku na kuhamisha mizigo kutoka kwenye treni. Binafsi nilikuwa na mizigo mingi na watoto wawili. Huku nanyeshewa mvua, nililazimika kukubaliana na hali halisi," alisema mmoja wa abiria hao, Jackline Jacob.

Treni hiyo iliwasili Dar es Salaam jana saa 5.15 asubuhi badala ya Jumanne asubuhi, kutokana na ajali mbili za treni, ikiwamo iliyotokea   Lukobe na kusababisha abiria kuhamishiwa kwenye mabasi.

"Kuna mizigo nimeibiwa kutokana na wingi wa watu na kutokuwa na ulinzi. Pia tulihanishwa usiku, kwa hiyo ulikuwa ni usumbufu wa hali ya juu. Kutoka tulikoteremkia hadi Morogoro Mjini pia ni mbali," alisema Josephine Cleophas wa Dar es Salaam.

Msemaji wa TRL, Midraj Maez akizungumzia tukio hilo, alisema hali hiyo ilitokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro na maeneo mengine nchini.

“Tulishazungumzia hilo pale Morogoro, lakini kifupi mvua ndiyo sababu ya tatizo hilo, lakini linafanyiwa kazi kurekebisha,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo