Wateja sugu wakatiwa umeme, Polisi imo


Mwandishi Wetu, Moshi

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kilimanjaro, limewakatia umeme wadaiwa sugu, likiwamo Jeshi la Polisi, wafanyabiashara, watu binafsi na idara za maji katika wilaya za Same na Mwanga.

Tanesco kwa sasa inawadai wateja wake zaidi ya Sh bilioni 15 huku wenye madeni makubwa wakiwa ni Polisi inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.1, Magereza Sh milini 400 na Maji Same na Mwanga Sh milioni 300.

Akizungumza jana na gazeti hili ofisini kwake, Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mahawa Mkaka, alisema shirika hilo limekuwa na operesheni mbalimbali na kubwa ikiwa ni ya kitaifa ya kukusanya madeni na kuwakatia umeme ambao hawajalipa.

Mkaka alisema wameendelea kufuatilia madeni hayo, ambapo Magereza walionesha nia ya kulipa na kurudishiwa huduma ya umeme, na ifikapo kesho watatakiwa wawe wamekamilisha mchakato wa kulipa deni lao.

Alisema Jeshi la Polisi nalo limeendelea na michakato ya kulipa deni lao, na kwamba wakiweka mikataba vizuri na kuonesha nia ya kulipa, watarejeshewa huduma ya umeme.

“Tanesco kwa sasa tumeendesha operesheni kama nne, na ya kwanza ni ya kitaifa ya kukusanya madeni na kuwakatia huduma ya umeme wateja ambao hawajalipa, mpaka sasa tumekata umeme kwa wateja mbalimbali zikiwamo taasisi za Serikali, kwani fedha tunazodai ni zaidi ya Sh bilioni 15, na ni endelevu mpaka wateja wote walipe  malimbikizo yao ya madeni ya ankara za umeme,” alisema Mkaka.

Aidha, Mkaka alisema Operesheni nyingine inayoendeshwa na shirika hilo mkoani Kilimanjaro, ni ya ukaguzi wa miundombinu ya umeme, ambayo ilitarajiwa kuanza jana kwa lengo la kumaliza tatizo la baadhi ya wananchi kujiunganishia umeme kinyume cha sheria na tatizo la wizi na uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo