Asilimia 90 wasichana wa wafugaji wakeketwa


Richard Mwangulube, Arusha

MAENDELEO ya elimu katika wilaya za wafugaji mkoani hapa, yamekuwa yakidhoofishwa na mila potofu za ukeketaji watoto wa kike   wakiwa shuleni na kuchangia taaluma kushuka.

Hali hiyo imesababisha maendeleo ya taaluma kutoridhisha na kusababisha kushuka kwa matokeo ambapo asilimia 90 ya wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari wamebainika kukeketwa.

Utafiti uliofanywa katika baadhi ya sekondari kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ulionesha kuwa asilimia 90 ya wasichana kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita wamekeketwa.

Hali hiyo ilielezwa kutokana na kuendelezwa mila potofu katika maeneo hayo ambayo asilimia kubwa ni ya wafugaji ambao wanaamini mtoto wa kike bila kukeketwa ni vigumu kupata mume.

Udhaifu wa kamati za maendeleo za kata na za shule unatajwa pia kuendeleza mila hiyo ya ukeketaji wasichana, jambo lililogeuka kuwa la kudumu katika jamii za wafugaji huku wakiendesha vitendo hivyo kwa kificho.

Kwa mujibu wa utafiti huo, katika kata ya Mwandeti, binti wa miaka 13 alikeketwa na kupoteza maisha kwa kupoteza damu nyingi na wazazi kumzika kisiri.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi lililazimika kufukua maiti   kwa ajili ya uchunguzi huku wazazi wakitorokea kusikojulikana  na hawajapatikana hadi sasa.

Utafiti huo unaonesha kuwa taarifa za baadhi ya wataalamu wa afya Mwandeti zinaonesha kuwa asilimia 90 ya wanafunzi wa kike wamekeketwa.

Taarifa hiyo inaonesha kwamba idadi kubwa ya watoto wa kike kupata mimba au kuolewa wakisubiri matokeo ya kidato cha kwanza na cha pili na utoro ni baadhi ya mambo yanayoathiri taaluma katika maeneo ya wafugaji.

Utafiti mwingine uliofanywa katika sekondari ya Musa katika Halmashauri ya Arusha, unaonesha kuwa hali ya ukeketaji bado ni kikwazo kwa elimu.

“Katika sekondari za Lengijave na Oldonyosambu idadi kubwa ya wasichana wamekuwa wakiacha masomo na kuozeshwa na wazazi wao hali ambayo imeathiri taaluma,” alisema mwalimu ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia usalama wake.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo