*Samia kuongoza watakaoaga miili ya marehemu leo
Suleiman Msuya
WAKATI miili ya wanafunzi 33 wa Shule ya
Msingi Lucky Vincent ikitarajiwa kuagwa leo mjini Arusha, makundi mbalimbali ya
mitandao ya kijamii ikiwamo WhatsApp yameungana kuomboleza msiba huo kwa kuweka
alama ya mishumaa.
Wanafunzi hao, walimu wao wawili na
dereva walifariki dunia juzi baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuingia
kwenye korongo na kupinduka eneo la Rhotia Kata ya Rhotia, Wilaya ya Karatu
mkoani Arusha.
Ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi hao
wa shule hiyo ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza iliyopo jijini Arusha
wakielekea kwenye mitihani ya ujirani, kujipima nguvu katika Shule ya Tumaini
English Medium.
Katika kile kilichoonesha ni kundi kubwa
kuguswa na tukio hilo, wanachama na viongozi wa makundi mbalimbali walipendekeza
kuwekwa kwa alama za mishumaa kwenye eneo maalumu la alama ya kila kundi ili
kuungana na wazazi na familia zilizopatwa na msiba huo.
Baadhi ya makundi ambayo yalibadilisha
alama au nembo zake na kuweka picha ya mshumaa ni Quality Media Group,
Wanahabari Tanzania, Maroro na Mikuyuni, Mawazo Huru, Endorsers of Kahangwa,
Wasomi wa MNMA, MNMA Great Thinkers na Events & Entertainment.
Mengine ni Sports HQ Tanuey la Fikra,
Jukwaa la MNMA, Tasnia ya Mawasiliano, MNH Talks Reloaded, Karagwe Yetu &
Friend, Kilimo Kwanza Group, Majirani Goba, Dar Young Africans, WCB,
Tukumbukane, United Redblood Fans, Vodacom PL Tanzania, Official WCB Group na
Yanga Whatsap Family.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan leo ataongoza wakazi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani
kuaga miili ya wanafunzi 33, wawili wawili na dereva wa Shule ya Lucky Vicent
waliopoteza maisha juzi baada ya gari kupata ajali kwenye eneo la Rhotia Kata
ya Rhotia, wilayani Karutu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Arusha, Mrisho
Gambo jana ambapo alibainisha kuwa utaratibu wa kuwaaga wapendwa hao utaanza
saa mbili asubuhi katika kiwanja cha Sheikh Amri Abeid.
Awali jana mkuu wa wa wilaya alitangaza
kuwa marehemu hao wataagwa jana lakini baadae ilitoka taarifa ya mabadiliko
ambalo leo wataagwa shughuli ikiongozwa na Makamu wa Rais Suluhu.
Aidha, inatarajiwa katika shughuli hiyo
ya kuuga viongozi mbalimbali wa dini, kisiasa, serikali na kijamii watashiriki
pamoja na familia kutoa salamu za mwisho.
Marehemu hao walikutwa na ummauti wakati
wakiwa safarini Karatu kufanya mtihani wa ujirani mwema na shule ya Msingi
Tumaini ambapo walikuwa na msafara wa gari tatu na gari moja ndio ilipata ajali
na kusababisha vifo vya watu 36.
Taarifa mbalimbali ambazo zilizopatikana
zinadai kuwa gari hiyo ilifeli breki kutokana na mvua inayoendelea kunyesha
wilayani hapo.
Vifo hivyo vimeacha simanzi kwa
Watanzania wengi huki ikisemekana mmoja wa wazazi ambaye watoto wake watatu
wamepoteza maisha alipoteza maisha baada ya tukio hilo.
Kutokana na tukio hilo watu mbalimbali
wameendelea kutuma salamu za maombelezo ambapo mmoja wapo ni Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye aliweka ujumbe unaosema ni
watoto wetu, ni wenzetu, hakika ni pigo kubwa sana kwetu, Mungu aziweke roho za
marehemu mahali peponi amina.
0 comments:
Post a Comment