*Walaumu iliyopita kushindwa kufikiwa kikamilifu
*Wasema ni kutokana
na Serikali inavyojiendesha
Sharifa Marira,
Dodoma
SERIKALI imewasilisha Sura ya Bajeti yake ya mwaka
2017/18 ikionesha jumla ya Sh bilioni 31,699.7 zinatarajiwa kukusanywa huku
wabunge wakiponda kuwa haitatekelezeka.
Wamesema hata bajeti iliyopita imeonekana kukwama
kutokana na namna Serikali inavyojiendesha.
Akiwasilisha sura hiyo jana kwenye ukumbi wa Bunge mjini hapa,
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema fedha hizo zinatarajiwa
kutoka vyanzo mbalimbali Sh bilioni 17,106.3 huku za kodi zikiwa ni Sh bilioni
2,183.4.
Alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh
bilioni 3,971.1 ambayo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote, ambapo Serikali inatarajia
kukopa Sh bilioni 6,156.7 kutoka soko la ndani.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliponda Serikali
kuongeza bajeti hadi zaidi ya Sh trilioni 31 wakati bajeti iliyopita
iliyokuwa Sh trilioni 29 ilishindwa kufikiwa kutokana na wadau wa maendeleo
kushindwa kuchangia.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (Act -Wazalendo)
alisema katika taarifa iliyowasilishwa na Dk Mpango, hadi Februari mapato
kutoka vyanzo vyote yalifikia Sh bilioni 15,372.4 sawa na asilimia 79 ya lengo
la kipindi hicho.
Alisema hali hiyo ilitokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya
kukosekana kwa mikopo yenye masharti nafuu, jambo alilosema lilitokana na
utendaji wa Serikali.
"Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa
maendeleo ilikuwa ni Sh bilioni 1,253.6 pekee na sababu ya hali hiyo ni wadau kukosa
imani na Serikali kwa matamko yake na kutoheshimu mikataba iliyowekwa na
Serikali zilizopita," alisema Zitto.
Alisema bajeti hiyo si halisia na jambo ambalo
haliwezekani kutekelezwa, ikiwa ya mwaka 2016/17 Serikali ilishindwa kufikisha Sh
trilioni 29 ya mwaka unaomalizika.
“Hiyo ya Sh trilioni 31 itafikiwa lini? Hadi sasa
ni asilimia 52 tu ya bajeti nzima ndiyo ilipatikana nayo haina uhalisia wowote
ni ya maandishi tu.
“Hata katika miradi ya maendeleo ambayo inadaiwa kutekelezwa
kwa asilimia 35 haijakidhi haja ya maisha ya Watanzania, kwani miradi
iliyotekelezeka ni ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli pekee, wananchi hawana
maji, barabara, umeme na huduma bora za afya," alisema na kuongeza:
"Kwa mara ya kwanza katika historia, Serikali
imeshindwa kukopa Sh. trilioni tano, hii ni kutokana na kutoaminika kwake.
Kumekuwa na utaratibu wa viongozi kutoa matamko yanayokinzana na mikataba
ambayo yanawaogofya wahisani, hivyo kupandisha riba ili tushindwe kukopa."
Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) alisema tatizo
lililopo ni Serikali kuweka bajeti ya kufikirika wasiyo na uhakika wa kuipata
na ndiyo sababu mara nyingi bajeti hazitekelezeki na wanashindwa kufikia
malengo.
Alisema hakuna haja kwa Serikali kuongeza nakisi ya
bajeti hadi Sh. trilioni 31 wakati katika bajeti inayoishia Juni wameshindwa
kutimiza lengo la Sh trilioni 29 iliyokuwa imekusudiwa.
"Tusiwe tunaweka bajeti za kujidanganya, ili mambo
yaende tuweke nakisi ambayo tuna uwezo wa kuifikia, ili mipango yetu iende sawa
haiwezekani kila siku tunalalamika kwamba bajeti haijatekelezeka wakati
tulikuja bungeni kuipitisha," alisema Mollel.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alisema Serikali
haijaeleza ni namna gani inakwenda kujenga uchumi wa viwanda, hakuna mahali
sekta ya kilimo imeonekana kama ndio msingi mkuu wa viwanda, hivyo haelewi kama
kuna viwanda bila kilimo.
Alisema katika nakisi hii ya bajeti inaonekana mapato ya
ndani yanatakiwa kuongezeka kutoka Sh trilioni 15 hadi 19 jambo ambalo linampa shaka
kwamba wananchi ndio watakaobebeshwa mzigo huo kwa kuongezwa kodi.
0 comments:
Post a Comment