Charity James
Obrey Chirwa |
KASUSIWA timu! Hivyo ndivyo unavyoweza
kusema kwa wale wapinzani wa timu ya Yanga mara baada ya mshambuliaji wa
kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa (pichani), kuwa ndiye mshambuliaji pekee
katika kikosi cha timu hiyo kilichoondoka kwenda kurudiana na Zanaco.
Yanga inatarajia kuwa mgeni wa Zanaco ya
Zambia katika mchezo wa marudiono wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo
katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo, Yanga itawakosa washambuliaji
wao wawili tegemeo, Donald Ngoma na Amisi Tambwe ambao wanasumbuliwa na
matatizo ya goti huku nafasi hiyo ikisalia kuwa mzigo kwa Chirwa ambaye ndiye
atakayeongoza jahazi hilo ugenini.
Endapo Yanga ikipata matokeo mazuri
katika mchezo huo, itakuwa imekata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya
michuano hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kocha
Msaidizi wa klabu hiyo, Juma Mwambusi alisema bado hawajakata tamaa kuelekea
mchezo huo pamoja na kukabiliwa na majeruhi wengi kwani wanaamini wana nafasi
ya kufanya vizuri.
‘’Yanga inawachezaji wengi na mifumo
huwa inabadilika, hivyo hatuna sababu ya kukata tamaa kwasababu ya kukosa
wachezaji wawili katika kikosi tuna imani tutafanya vizuri na kuendelea katika
hatua nyingine bila ya wachezaji hao,’’ alisema.
Alisema Ngoma na Tambwe ni wachezaji wazuri
na wana umuhimu katika kikosi lakini kukosekana kwao haina maana kuwa watashindwa
kufanya vizuri katika mchezo huo ambao ni muhimu kwao kuhakikisha wanafanya vizuri
ili waweze kuendelea katika hatua nyingine.
Mbali na wachezaji hao, wengine
watakaokosa mchezo huo ni mshambuliaji Matheo Anthony, Ben Kakolanya, Pato Ngonyani,
Malimi Busungu na Yusuph Mlilo.
Yanga haina budi kupata ushindi au
sare ya kuanzia mabao 2-2 ndipo ikate tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya
michuano hiyo na endapo itatolewa itaangukia katika Kombe la Shirikisho kama
ilivyokuwa mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment