Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Dk Shein |
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Juma Abadallah Sadallah ‘Mabodi’, amewataka watendaji wa chama hicho kufanya
kazi kwa pamoja ili kufanikisha azma ya mageuzi yaliyofanywa ndani ya chama
hicho hivi karibuni.
Akizungumza na watendaji hao baada ya
kukabidhiwa rasmi ofisi tangu ateuliwe kushika wadhifa huo wiki iliyopita,
alisema viongozi wanapaswa kuwa sehemu ya mageuzi hayo ili kuleta tija kwa wananchi
wote.
Sadallah ambaye aliwahi kuwa Naibu
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika serikali ya awamu ya nne,
alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha umoja na maelewano miongoni mwa jamii licha
ya kuwepo kwa tofauti za kiitikadi.
Aliwataka kufuatilia kwa karibu utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015 hadi 2020 unaofanywa na serikali zote mbili
ili kuwaondolea wananchi kero zinazowakabili na kwamba, hatamvumilia kiongozi
au mtendaji atakayeshindwa kutekeleza maelekezo yanayotolewa na chama na
serikali.
“Naomba tuendelee kushirikiana katika
maandalizi ya uchaguzi wa dola wa mwaka 2020 kwa kuzisimamia serikali
zitekeleze ilani ya uchaguzi ya chama chetu na tutakapoona kasi hairidhishi
tutatekeleza kwa kutumia rasilimali za chama ilimradi wananchi wetu wasipate
tabu,” alisema Mabodi.
Akizungumzia mikakati ya kukiimarisha
chama, Naibu huyo alieleza kuwa, mbali ya kutumia nyenzo mbalimbali
alizokabidhiwa na mtangulizi wake, Vuai Ali Vuai, alisema atatumia busara na hekima
ili kuhakikisha chama hicho kinaongeza wanachama wanaokiunga mkono.
“Mtaji wa chama siku zote ni
wanachama, jukumu langu na lenu kuhakikisha tunatumia mbinu mbalimbali za
kuongeza wanachama na hatutaweza kufanya hivyo kama hatutawafuata mahali walipo,”
alisema mbunge huyo wa zamani wa Rahaleo, Unguja.
Akizungumzia namna atakavyosaidia
kukuza ajira kwa vijana, alieleza kuwa mbali ya kusimamiwa kwa utekelezaji wa
sera na mikakati mbalimbali na serikali, CCM itaanzisha na kuviendeleza vyuo
vya amali ili kuongeza idadi ya watu wanaojiajiri.
Alisema mbali ya hatua hiyo kusaidia
kupunguza tatizo la ajira, pia itasaidia kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali
watakaotumika katika viwanda vitakavyoanzishwa nchini kutokana na utekelezaji
wa sera ya uchumi wa viwanda inayotekelezwa na serikali zote mbili za Tanzania.
“Hatuwezi kuingia katika uchumi wa
viwanda bila ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi mzuri, pamoja na serikali
kutekeleza mikakati ya kukuza uchumi na chama kitafanya hivyo, si kwa lengo la kupunguza
ajira tu, bali kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na tabia ya kuwa omba omba,”
alisema Mabodi.
Akizungumzia hali ya amani na utulivu
nchini, alisema atakuwa mstari wa mbele kuilinda Amani iliyopo na hatasita
kukaa na mtu au kikundi chochote ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumu nchini.
“Nitatumia nguvu na uzoefu wangu wote
kuhakikisha nchi inabaki salama hata kwa kuzungumza na watu ambao watakuwa wanaonekana
kuwa na nia ya kuvuruga amani ya nchi yetu.
Hili nitalifanya kwa manufaa ya watu
wetu ambao ndiyo waathirika wakubwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment