Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Julius Mtatiro |
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimepinga hatua ya Serikali kuipa
madaktari Kenya, badala yake kimeitaka kuhakikisha inaimarisha huduma za afya
kwa wananchi wake.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya juzi Rais John Magufuli
kutangaza kuipa Kenya madaktari 500 ili wakafanye kazi nchini humo baada ya madaktari
wa nchi hiyo kugoma kwa muda mrefu sasa.
Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la
CUF, Vuga mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa muda wa chama
hicho, Julius Mtatiro, alisema uamuzi wa Rais Magufuli haupaswi kutekelezwa
kutokana na ukweli kwamba Tanzania ina mahitaji makubwa ya madaktari maeneo mbalimbali.
Mtatiro alisema hata kama ingelikuwa Tanzania imejitosheleza kwa
wataalamu na uimara wa huduma za afya kwa watu wake, sasa si wakati mwafaka
kupeleka madaktari nchini Kenya kutokana na kutetereka kwa uhusiano kati ya
watumishi wa sekta hiyo na serikali ya nchi hiyo.
Mtatiro alieleza kuwa madaktari wa Kenya wamehoji sababu za
serikali yao kuomba msaada wa madaktari 500 wakati huu wakati wao wamemaliza
mgomo jambo linaloashiria kutokubalika kwa watendaji hao.
“Kila mmoja anajua lililokokea Kenya muda huu, madaktari wana mgogoro
na serikali, vipi wanachukuliwa madaktari wetu kupelekwa huko bila ya
kuhakikishiwa usalama wao?“ alihoji mwenyekiti huyo. Alieleza kuwa Tanzania ina
upungufu wa madaktari 3,330 wanaoweza kuhudumia wananchi 8,000 hivyo bado
Tanzania inahitaji kuajiri madaktari zaidi hasa katika maeneo ya mikoani.
“Inashangaza kuona wanawake wanakufa kwa ajili ya uzazi kutokana na
kukosa madaktari au huduma stahiki za afya, lakini serikali inakubali kwa
mbwembwe kupeleka madaktari katika nchi nyengine jambo ambalo kwa akili za
kawaida tu halikubaliki”, alieleza Mtatiro.
Akizungumzia suala la uchumi alieleza kuwa umeendelea kudorora na
wananchi kuwa na hali mbaya ya uchumi jamboa ambalo ni tofauti na katika awamu
iliyopita.
“Katika awamu iliyopita serikali ilikuwa ikikusanya wastani wa
shilingi bilioni 800 kwa mwezi lakini ilikuwa na uwezo kupeleka fedha katika
maeneo ya utendaji” alieleza.
Alidai kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John
Mugufuli inakusanya Sh. trilioni 4.5 kwa mwezi, lakini inashindwa kupeleka fedha
za kutosha katika sekta za huduma za jamii na kiasi kikubwa kuelekezwa kwenye
ulipaji wa mishahara na madeni bila ya kuzingatia uwiano wa utoaji wa fedha za
maendeleo na matumizi ya kawaida.
Mtatiro aliwataka wabunge wa chama chama hicho lazima wahakikishe wanafanya
kazi ya kuibana serikali ili kuhakikisha inaimarisha uchumi kwa maslahi ya taifa.
Mkutano huo wa siku moja ulikutana mjini Unguja kujadili mambo mbali
mbali yanayohusu chama hicho na taifa kwa ujumla kilihudhuriwa pia na katibu
mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad sanjari na wajumbe wa baraza hilo
waliotangazwa kuvuliwa nafasi zao na Mwenyekiti wa chama hicho anaetambuliwa na
ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Profesa Ibrahim Haroun Lipumba.
0 comments:
Post a Comment