Rais John Magufuli |
UAMUZI wa Rais John Magufuli kuzuia
mchanga wa dhahabu kusafirishwa nje ya nchi umewaathiri wachimbaji wadogo.
Wachimbaji hao jana walimpigia magoti
Mkuu huyo wa Nchi wakieleza kuwa hali hiyo imesababisha wapate hasara, huku
mamia ya wananchi wakikosa ajira.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam, wachimbaji hao sita wa madini ya aina mbalimbali waliozungumza kwa
niaba ya wenzao, walisema licha ya lengo zuri la Rais, uamuzi wa kuwabana hata wao
ambao hawachimbi dhahabu lakini wanasafirisha mchanga wenye
madini mengine, unapaswa kuangaliwa upya.
Kwa mujibu wa wachimbaji hao, hadi jana kontena
zao zaidi ya 60 zimezuiwa maeneo mbalimbali nchini huku wakilazimika kulipa Sh 45,000
kwa siku kwa kila kontena, huku wakishauri yaachwe hayo pamoja na yaliyoko
bandarini ili kusaidia wasipate hasara.
Hadi Jumapili kontena 282 zenye mchanga
wa dhahabu zilikuwa zimezuiwa kwenye bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni takribani
siku tano tangu Rais Magufuli ashuhudie kontena 20 zenye mchanga huo.
Rais alizuia kusafirishwa kwa mchanga
huo na kuwekwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama katika hatua ambayo Bunge liliingilia
kati na kuunda timu ya uchunguzi wa biashara ya madini nchini, huku Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa uteuzi wake
ukitenguliwa.
“Mimi ni mchimbaji na msafirishaji wa madini ya nikeli. Nimeathirika na zuio la
Rais Magufuli kwa sababu nimesimamisha shughuli zangu na kusitisha ajira kwa
wachimbaji wangu.
“Kifupi nimefilisika maana kontena zangu
13 ilikuwa nizisafirishe nimeshindwa bado ziko mgodini Mpwapwa, Dodoma, “ alisema Thobias Rweyemamu,
Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Metali.
Rweyemamu alisema akisitisha shughuli
mgodini mwake kwa siku moja anaingia hasara ya Sh milioni 4, na sasa amesitisha
uchimbaji kwa takribani mwezi mmoja.
King Seleman ambaye anachimba madini ya metali
pekee alisema, “migodi mingi tunayopata kutoka wizara ya madini ni ya shaba na
kutokana na kiwango kidogo cha madini hayo na mengine, ndiyo maana hakuna
mwekezaji anayeweka kiwanda.”
Alisema wenye migodi ya dhahabu
wanafaidika kwa sababu huambatana na madini ya shaba na fedha na kusisitiza
kuwa wanapozuiwa kusafirisha mchanga wenye shaba na madini mengine wanaathirika
huku akidai zuio la Rais linahusu wachimbaji wakubwa.
“Sisi ni wamachinga katika sekta ya
madini. Ni kama wamachinga walio Kariakoo. Rais atufikirie,” alisema.
Mohamed Mkwayu ambaye ni mchimbaji mdogo
wa shaba alisema, “zuio linakosesha wafanyakazi mshahara na sisi tumesitisha
kuchimba maana hakuna pa kuupeleka mchanga. Rais ametuumiza kwa kweli, sisi
tunachimba shaba si dhahabu.”
Paul Kalyembe anayechimba shaba, garena na
zinki alisema wanalipa leseni ya Sh milioni 14 kuchimba madini hayo, tayari
wameshalipa na kumtaka Rais alegeze uamuzi wake.
0 comments:
Post a Comment