Suleiman Msuya
Mange Kimambi |
JENGO maarufu la kampuni ya Triz Motel Limited linalodaiwa
kumilikiwa na familia ya Mtanzania aishiye Marekani, Mange Kimambi ni miongoni
mwa nyumba na viwanja 10 vilivyotangazwa kuuzwa kwa mnada na Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Katika tangazo lake la juzi la mnada utakaofanywa na Wakala wa
Serikali, Kampuni ya Msolopa, Wizara hiyo iliwataka wananchi kujitokeza kununua
mali hizo za wadaiwa.
Mange aliyejipatia umaarufu kwa kuwa mchangiaji na mkosoaji wa mwenendo
wa Serikali ni mtoto wa marehemu John Kimambi ambaye anatajwa kuwa mmiliki wa
nyumba hiyo iliyoko Kinondoni.
Katika mnada huo ambao unatarajiwa kufanyika Machi 25 hadi Aprili mosi
unahusu pia wadaiwa Highland Estates Limited, Universal Electronics and Hard
Work, Bingo Simba Magwila, Zein Mohamed Baharoon na Camel Developers (T)
Limited ambaye anadaiwa viwanja vitano.
Wadaiwa hao wanamiliki viwanja namba 479 Mbezi, 102 Mbezi, 46/1A/C
Pugu , 2165 Mbezi , 79 na 86 Gerezani, 40 Kimbiji, 12-58 Temeke Mwanamakuru, 11
Mwanamakuru, 22 Aman Gomvu na 21 Aman Gomvu.
Kulingana na tangazo hilo, mnunuzi atapaswa kulipa asilimia 25
baada ya nyundo ya dalali na salio kulipwa ndani ya siku 14 huku anayeshindwa
kulipa akipoteza haki na gharama za kuhamisha ununuzi zitakuwa juu ya mnunuzi.
Akizungumzia kiwanja hicho kwenye mitandao ya kijamii, Mange
alidai Magufuli (Rais John) ameamua kuuza eneo lake la familia ambalo anamiliki
asilimia 25 ya hisa.
Alisema familia yake haijui kuhusu deni linalohusishwa na nyumba
hiyo na kwamba yeye ndiye aliwaambia ndugu zake kwa ujumbe kuwa nyumba yao
inauzwa “Eti tunadaiwa ardhi,” alisema na kuongeza: “Yaani ni kichekesho cha
mwaka … hawana barua hata moja ya kuambiwa wakalipe chochote Ardhi.
Na nilihakikisha wanalipa kodi vizuri ili tusimpe sababu.” Kupitia
mitandao ya kijamii Mange aliandika: “Wewe uza mpaka nyumba za babangu zote,
fanya lolote lile muhimu tu utaniacha ….”
0 comments:
Post a Comment