Hastin Liumba, Kahama
Profesa Palamagamba Kabudi |
WAZIRI wa Katiba
na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais John
Magufuli ameombwa kuanza kazi yake kwa kufufua ajenda ya Katiba Mpya inayogusa
maslahi mapana ya Taifa.
Ushauri huo
umetolewa na Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation, taasisi
inayoshughulikia utawala bora na haki, Khamis Mgeja wakati akizungumza na waandishi
wa habari wilayani hapa juzi kuhusu mustakabali wa Taifa.
Alisema suala la
Katiba Mpya si la kikundi, wala mtu hivyo akashauri mawazo ya wananchi
yaheshimiwe.
“Namtambua
Profesa Kabudi kuwa ni msomi aliyebobea katika sheria, tunamwomba uzoefu wake
wa masuala ya sheria amshauri kwa umakini Rais Magufuli kuhusu matakwa ya
wananchi ya kupata Katiba mpya,” alisema.
Alisema ni vema Waziri
akatumia fursa hiyo kumshauri Rais Magufuli kuhusu Katiba Mpya sasa ili
mchakato wa kupatikana kwake uanze tena na hatimaye ufikie tamati.
Mgeja alisema
bahati nzuri Profesa Kabudi alikuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba na kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa
rasimu iliyotokana na matakwa na maoni ya wananchi.
“Waziri atumie
fursa hiyo na tuna imani suala hilo la Katiba Mpya sasa kama ni upele umepata
mkunaji,” alisema Mgeja.
Hata hivyo, aliihadharisha
Serikali isije kutafuta visingizio katika kutekeleza suala hilo na kwamba shaka
yao ni visingizio kuwa muda hautoshi kufanya mchakato wa Katiba Mpya.
Mgeja alisema
zaidi ya Sh bilioni 300 zilitumika kwenye mchakato huo na ikiwa hakuna umuhimu
wa suala hilo, fedha hizo zingetumika katika huduma zingine za jamii kama afya,
maji, ujenzi wa miundombinu au kununua chakula cha akiba na njaa.
Aliikumbusha Serikali
ya Awamu ya Tano kwamba suala hilo la Katiba Mpya lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015/20 na chama hicho kimeingia mkataba na Watanzania kuwaongoza,
hivyo wana deni kubwa kwa wananchi kuwapa Katiba Mpya.
0 comments:
Post a Comment